Jeshi la Sudan ladhibiti maeneo ya Khartoum na kulenga ikulu ya rais
Duru za habari zimekinukuu chanzo kimoja nchini Sudan kwamba jeshi la nchi hiyo limeshambulia ikulu ya rais mjini Khartoum kwa ndege zisizo na rubani na kudhibiti maeneo ya katika mji mkuu, ambayo baadhi bado yako chini ya udhibiti wa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Duru hizo zimeiripoti kwamba shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye ikulu ya rais limesababisha uharibifu wa vifaa vya kivita, na kwamba wapiganaji wa Rapid Support Forces walionekana wakiondoka kuelekea Jumba la Makumbusho la Sudan.
Eneo la katikati mwa Khartoum linashuhudia mapigano makali kati ya vikosi vya jeshi la taifa na wapiganaji wa RSF hususan karibu na Suuq al Arabi.
Duru za habari zinasema, jeshi la Sudan limedhibiti kituo cha Sharoni katikati mwa Khartoum, pamoja na vitongoji vya Khartoum 2 na Al-Usrah Club.
Wakati huohuo, duru hizo zimeripoti kuwa jeshi la Sudan limeuteka tena mji wa Abu Arif katika Jimbo la Sennar, kusini mashariki mwa Sudan.
Matukio haya yanakuja saa chache baada ya Kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), kuonekana kwenye rekodi mpya ya video, akiapa kuendeleza mapambana na jeshi la Sudan licha ya vikwazo vinavyokikabili kikosi hicho katika wiki za hivi karibuni katika maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na Khartoum na Jimbo la Al-Jazirah.