Angola yataka kusitishwa mapigano kabla ya mazungumzo ya amani DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124002-angola_yataka_kusitishwa_mapigano_kabla_ya_mazungumzo_ya_amani_drc
Rais wa Angola, João Lourenço, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) ametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano katika mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
(last modified 2025-03-16T22:55:14+00:00 )
Mar 16, 2025 22:55 UTC
  • Rais wa Angola, João Lourenço
    Rais wa Angola, João Lourenço

Rais wa Angola, João Lourenço, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) ametoa wito wa kusitishwa mara moja mapigano katika mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Lourenço amezitaka pande zote husika katika mzozo wa mashariki mwa Kongo kusitisha mapigano kuanzia usiku wa manane wa leo kwa saa za huko katika juhudi za kuandaa anga ya maelewano kuelekea mazungumzo yayajo ya amani. 

Taarifa kutoka Ofisi ya Rais wa Angola imeeleza kuwa, usitishaji vita unaopaswa kutekeleza ni lazima ujumuishe hatua zote za uhasama na mashambulizi dhidi ya raia na kusitisha vitendo vyote vya kuteka maeneo mapya huko mashariki mwa Kongo.

Mazungumzo ya amani ya Kongo yamepangwa kufanyika Luanda mji mkuu wa Angola tarehe 18 mwezi huu wa Machi; ambapo serikali ya Kinshasa na waasi wa kundi la M23 watakutana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu. 

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hadi sasa haijathibitisha rasmi kama itashiriki katika mazungumzo hayo au la. Hata hivyo, imeelezea kuunga mkono mpango wa amani wa Angola na kumtaka Rais Felix Tshisekedi kujitolea waziwazi kuongoza mazungumzo.

Mzozo umeongezeka hivi karibuni mashariki mwa Kongo, ambapo waasi wa M23 waliteka miji muhimu katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini, na kuwalazimisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao. Licha ya juhudi za kidiplomasia, makabiliano kati ya vikosi vya jeshi la serikali ya DRC na waasi wa M23 yanaendelea, na hivyo kudhihirisha udharura wa kufanyika mazungumzo baina ya pande mbili.