Waziri wa Elimu Libya atupwa jela miaka 3.5 kwa ubadhirifu
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Libya imetangaza kwamba Waziri wa Elimu wa nchi hiyo, Musa al-Magaryaf, amehukumiwa kifungo cha miaka 3.5 jela kwa ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Mashtaka hayo yanatokana na waziri huyo kuhusika katika kusimamia taratibu za ukandarasi wa uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya shule. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Libya imesema kwamba al-Magaryaf alikiuka kanuni ya usawa na alifanya upendeleo na ubaguzi wakati wa kutoa kandarasi ya uchapishaji vitabu.
Uamuzi wa mwisho wa mahakama hiyo umejumuisha kifungo cha miaka 3.5 jela, faini ya dinari 1,000 za Libya (takriban dola 207 za Kimarekani), na kunyimwa haki za kiraia kwa muda wa kifungo hicho ambako kutaenelea kwa mwaka mmoja wa ziada baada ya kutumikia kifungo.
Sehemu moja ya taarifa ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Libya imesema: Mahakama imempata na hatia al-Magaryaf kutokanaa na uhaba wa vitabu vya kusomeshea tangu mwaka 2021.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa mwaka wa shule wa 2021, ambapo uhaba wa vitabu uliwalazimimisha wazazi kutumia pesa kununua vitabu ambavyo vilivyopaswa kutolewa bure katika skuli za umma.
Kwanza Magaryaf aliwekwa chini ya uchunguzi kuhusu usimamizi wake wa taratibu za kimkataba za uchapishaji wa vitabu na halafu aliwekwa kizuizini kama sehemu ya uchunguzi wa kashfa hiyo.
Baadaye Magaryaf aliachiliwa huru kutoka kizuizini kwa kukosekana ushahidi, na alirejea kwenye nafasi yake ya Waziri wa Elimu. Lakini juzi Jumapili, Mwanasheria Mkuu wa Libya alitangaza kwenye Facebook kwamba Magaryaf ametiwa nguvuni na amehukumiwa kifungo cha miaka 3.5 jela.