RSF: Hatutoondoka Khartoum, Jeshi ndilo lililojitoa kwenye mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124046-rsf_hatutoondoka_khartoum_jeshi_ndilo_lililojitoa_kwenye_mazungumzo
Kamanda wa Vikosi vya Msaada wa Haraaka RSF vya Sudan amelilaumu jeshi la nchi hiyo SAF kwa kukwamisha mazungumzo ya amani nchini humo na kusema kuwa, askari wake hawataondoka mjini Khartoum.
(last modified 2025-03-17T22:43:17+00:00 )
Mar 17, 2025 22:43 UTC
  • RSF: Hatutoondoka Khartoum, Jeshi ndilo lililojitoa kwenye mazungumzo

Kamanda wa Vikosi vya Msaada wa Haraaka RSF vya Sudan amelilaumu jeshi la nchi hiyo SAF kwa kukwamisha mazungumzo ya amani nchini humo na kusema kuwa, askari wake hawataondoka mjini Khartoum.

Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la Hemedti amesema hayo kwenye hotuba aliyoitoa kwa njia ya televisheni na kuongea kuwa, vikosi vilivyoko chini ya uongozi wake havitaondoka Khartoum na wala havitaacha nafasi zao.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Russia la Sputnik, kamanda huyo wa "Vikosi vya Msaada wa Haraka" (RSF) amesema: "Tulifanya kila kitu kuzuia vita na tulikwenda Jeddah kwa nia ya dhati na tukatia saini Mkataba wa Jeddah, tukiwa na nia ya dhati ya kufikia suluhisho la kisiasa la mgogoro uliopo."

Jenerali Hemedti pia amesema: "Tulishiriki kwa umakini na uaminifu katika mazungumzo ya Manama ili kusaini makubaliano juu ya mfumo wa madaraka unaokubaliwa kimataifa, lakini mkuu wa timu ya mazungumzo wa SAF alitoweka siku moja kabla ya kuchunguzwa na kujadiliwa ya rasimu ya makubaliano hayo, na baada ya hapo ujumbe wa jeshi uliomba radhi na kujiondoa kwenye makubaliano ya Manama."

Vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan vimekuwa vikiendelea tangu katikati ya mwezi Aprili 2023 kati ya pande mbili hasimu yaani Jeshi la Sudan (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vinavyoongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo maarufu kwa jina la Hemedti.