UN: Vita Ituri DRC vimepelekea watu 100,000 kuwa wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124058-un_vita_ituri_drc_vimepelekea_watu_100_000_kuwa_wakimbizi
Umoja wa Mataifa unaripoti kuwa mapigano ya silaha katika jimbo la Ituri, Kaskazini-Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), yamesababisha watu takriban 100,000 kufurushwa kutoka makazi yao. Mapigano kati ya kundi la waasi wa M23 na Jeshi la Serikali ya DRC (FARDC) pia ni chanzo kuongezeka idadi ya wakimbizi katika jimbo la Kivu Kusini.
(last modified 2025-03-18T04:18:54+00:00 )
Mar 18, 2025 04:18 UTC
  • UN: Vita Ituri DRC vimepelekea watu 100,000 kuwa wakimbizi

Umoja wa Mataifa unaripoti kuwa mapigano ya silaha katika jimbo la Ituri, Kaskazini-Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), yamesababisha watu takriban 100,000 kufurushwa kutoka makazi yao. Mapigano kati ya kundi la waasi wa M23 na Jeshi la Serikali ya DRC (FARDC) pia ni chanzo kuongezeka idadi ya wakimbizi katika jimbo la Kivu Kusini.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), ghasia katika maeneo ya Djugu, Irumu, na Mambasa zimesababisha vifo vya zaidi ya raia 200 kati ya Januari na Februari 2025, wakiwemo wanawake na watoto, huku wengine wengi wakijeruhiwa. Vurugu hizo pia zimekuwa zikishuhudiwa katika vijiji kama Fataki, Drodro, na Tchomia.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu, mpango wa Umoja wa Mataifa nchuni DRC, MONUSCO, umesema waasi wa M23 wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya kijeshi mashariki mwa DRC kwa msaada wa jeshi la Rwanda na wamechukua udhibiti wa sehemu kubwa za majimbo ya Kaskazini na Kusini mwa Kivu.

OCHA imeonya kuwa  vurugu inasababisha nchi hiyo ya Maziwa Makuu kushuhudia moja ya migogoro migumu zaidi ya kibinadamu duniani, huku zaidi ya watu milioni 21 wakiwa na mahitaji mengi.

Aidha OCHA imetahadharisha kwamba mapigano haya makali yamelazimisha mamia ya maelfu ya watu kuhama makazi yao na kuathiri utoaji wa huduma za msingi, jambo linaloongeza hatari ya kuenea magonjwa yanayohusiana na maji, kama vile kipindupindu.

Kati ya Januari na mapema Machi 2025, Umoja wa Mataifa umesema jiji la Goma limekuwa kitovu kipya cha mlipuko wa kipindupindu, likichangia asilimia 68 ya visa 1,846 vilivyoripotiwa katika kipindi hicho katika jimbo lote la Kivu Kaskazini.

Tayari likiwa janga sugu katika majimbo kadhaa ya nchi, OCHA imesema kuenea kwa haraka kunachochewa na hali duni ya maisha ya jamii zilizoko hatarini, zinazokabiliwa na vurugu na umaskini uliokithiri.