Aug 01, 2016 13:41 UTC
  • Nigeria kupambana na ukatili wa kijamii dhidi ya wanawake

Waziri wa Masuala ya Wanawake na Ustawi wa Jamii nchini Nigeria amesisitizia juu ya udharura wa kukabiliana na ukatili wa kijamii dhidi ya wanawake nchini humo.

Aisha Jummai Al-Hassan ameyasema hayo katika jimbo la Taraba ambalo asilimia kubwa ya wanawake wanakabiliwa na vitendo vya ukatili.

Huku akizindua vituo sita vya kufuatilia kesi hizo dhidi ya wanawake amelaani vikali mienendo hiyo ya ukandamizaji dhidi ya jamii hiyo. Al-Hassan amesema kuwa, katika kuhitimisha vitendo hivyo serikali imeazimia kusimamia haki za wanawake katika jamii.

Waziri huyo wa Nigeria ameyasema hayo katika hali ambayo vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake vimeongezeka sana nchini humo kutoka kwa wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram.

Waziri wa Masuala ya Wanawake na Ustawi Nigeria, Aisha Jummai Al-Hassan

Itakumbukwa kuwa mwezi April mwaka huu, wanachama wa kundi hilo sanjari na kushambulia vijiji vya Kuda katika jimbo la Adamawa, waliwaua kwa mazingira ya kutisha wakazi wa vijiji hivyo.

Saa chache baada ya hujuma hiyo, miili ya wanawake 18 iliokotwa eneo la tukio. Aidha wanawake wengine kadhaa walitoweka baada ya hujuma hiyo, ambapo inaamini wa kuwa walitekwa nyara na wanachama wa genge hilo maarufu kwa kutenda jinai.

wanachama wa Boko Haram

Hivi karibuni Benki ya Dunia ilitangaza kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram la nchini Nigeria hadi sasa wameua watu zaidi ya 20 elfu na kusababisha hasara ya dola bilioni 5.9 katika jimbo la Borno. Aidha ripoti hiyo ilisema zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa kundi hilo la Boko Haram.

Tags