M23: Hatutaki kingine ghairi ya amani nchini Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124122-m23_hatutaki_kingine_ghairi_ya_amani_nchini_kongo_dr
Muungano wa Mto Congo (AFC) na tawi lake la waasi wa M23 zinasisitiza kuwa, lengo lao kuu ni amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini zinadai kuwa, kufikiwa kwake kunakwamishwa na mashambulizi ya serikali.
(last modified 2025-10-21T03:09:04+00:00 )
Mar 20, 2025 03:09 UTC
  • M23: Hatutaki kingine ghairi ya amani nchini Kongo DR

Muungano wa Mto Congo (AFC) na tawi lake la waasi wa M23 zinasisitiza kuwa, lengo lao kuu ni amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini zinadai kuwa, kufikiwa kwake kunakwamishwa na mashambulizi ya serikali.

Katika mahojiano na Russia Today, msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka amesisitiza kuwa, mara kwa mara kundi hilo limetoa wito wa mazungumzo ya moja kwa moja na serikali ya DRC kutatua mzozo wa muda mrefu mashariki mwa nchi hiyo.

Kanyuka amesema licha ya juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Rais wa Angola Joao Lourenco, vikosi vya serikali vimeendelea kufanya mashambulizi kwenye maeneo yenye watu wengi, na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao.

Msemaji huyo wa M23 amesisitiza kuwa, vuguvugu hilo linapigania "kuwakomboa" watu wa Kongo kutoka kwa matamshi ya chuki, chuki dhidi ya wageni, ufisadi na utawala mbovu.

Msemaji wa M23, Lawrence Kanyuka

"Tuna madini mengi na utajiri mwingi chini ya ardhi ya DRC na idadi ya watu wetu hawanufaiki nayo," amesema Lawrence Kanyuka, msemaji wa M23.

Hii ni katika hali ambayo, mazungumzo baina ya waasi hao wa M23 na serikali ya DRC, yaliyopangwa kufanyika juzi Jumanne huko Luanda, mji mkuu wa Angola, yalikwama baada ya kundi hilo la waasi kusema halitoshiriki.