Mashambulizi ya Marekani Yemen yavuruga uuzaji wa chai ya Kenya
Biashara ya chai ya Kenya imeingia matatani baada ya Marekani na Uingereza kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Yemen na kupelekea jeshi la Yemen kujihami na kujibu uvamizi wa madola hayo ya kibeberu.
Marekani imeanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Yemen na kufanya jinai nyingine ya kivita nchini humo ili kuusaidia utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umeanzisha jinai mpya dhidi ya raia huko Ghaza na kukanyaga makubaliano yote yaliyofikiwa ya kukomesha jinai zake hizo.
Jeshi la Yemen nalo limeamua kulipiza kisasi kwa kushambulia meli za kivita za Marekani kwenye Bahari Nyekundu suala ambalo limepelekea vyombo vingine vya baharini kuogopa kupita kwenye eneo hilo la vita na kutatiza biashara zao.
Miongoni mwa walioathiriwa na uchokozi huo wa Marekani na Uingereza nchini Yemen ni sekta ya chai ya Kenya ambayo inasafirisha bidhaa zake kuelekea kwenye masoko muhimu ya barani Ulaya na Afrika Kaskazini kwa kutumia Bahari Nyekundu. Hayo yamethibitishwa pia na Bodi ya Chai ya Kenya (TBK).
TBK imesema katika ripoti yake iliyotolewa mjini Nairobi, kwamba mashambulizi hayo yamezua changamoto za upatikanaji wa soko kwa mauzo ya chai ya Kenya na kulazimisha meli kuchukua njia ndefu hadi kufika zinakokusudia.
Jeshi la Yemen limesema linashambulia tu vyombo vya Israel na Marekani na kila chombo kinachopeleka bidhaa kwa utawala wa Kizayuni, halishambulii vyombo vingine, lakini wafanyabiashara wana wasiwasi na mali zao kupita kwenye eneo la vita.
Mauzo ya chai ya Kenya mwaka jana 2024 yalifikia shilingi bilioni 181.6 (kama dola bilioni 1.4 za Kimarekani). Mwaka wa kabla yake yaani 2023 mauzo hayo yalikuwa ya dola bilioni 1.39.
Pakistan, Sudan, Misri, Uingereza na Yemen ni baadhi ya masoko ambayo yalirekodi kupungua uuzaji wa chai ya Kenya mwaka 2024.
Bodi ya Chai ya Kenya (TBK) imesema kuwa ina mikakati ya kupanua soko la chai ya Kenya kupitia shughuli maalumu za biashara kwa nchi kama vile Falme za Kiarabu, Iran, Uturuki, Ghana, Ujerumani na China.