Nchi Zaidi za Afrika zajiondoa katika Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa
Burkina Faso na Mali zimejitoa kutoka Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa (OIF), zikifuata mfano wa jirani wao wa Magharibi mwa Afrika, Niger, ambayo ilitangaza mapema kuondoka kwenye kundi hilo lenye makao yake mjini Paris.
Serikali ya Burkina Faso imesema kuwa OIF imepoteza mwelekeo wake wa awali wa kukuza ushirikiano wa kitamaduni na kiufundi, na kuwa chombo chenye upendeleo cha "ghiliba ya kisiasa."
Taarifa iliyosambazwa kupitia Shirika la Utangazaji la Burkina Faso AIB siku ya Jumatano imesema," Burkina Faso haiwezi kuendelea na ushirikiano na taasisi ambayo haiwezi kutimiza matarajio yake halali kuhusu haki, usawa, na uwazi."
Mapema wiki hii, Niger ilisema kuwa "imeamua kwa uhuru kujiondoa kutoka Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa," bila kueleza sababu za hatua hiyo. Nchi hiyo ya Sahel ilikuwa imesitisha ushirikiano wote na OIF kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya Julai 2023, ikilaumu shirika hilo kuwa chombo cha kisiasa cha kutetea maslahi ya serikali ya Ufaransa.
Jioni ya Jumanne, Mali, ambayo kwa sasa inaongoza urais wa Muungano wa Nchi za Sahel (AES) – kundi jipya lililoanzishwa na Burkina Faso, Mali na Niger – ilitoa taarifa ikitangaza uamuzi wa kuondoka "nchi wanachama wa muungano wa AES" kutoka umoja wa Kifaransa.
Dhamira iliyotangazwa ya OIF ni kukuza lugha ya Kifaransa, kusaidia amani na demokrasia, na kukuza elimu na maendeleo katika nchi zinazozungumza Kifaransa duniani, nyingi ambazo zilikuwa koloni za Ufaransa zamani.

Baraza la Kudumu la kundi hilo lenye wanachama 88 lilisitisha uanachama wa Mali, Burkina Faso, na Niger kufuatia mapinduzi ya kijeshi katika nchi hizo tatu ambazo zilikoloniwa na Ufaransa na ambazo zilikuwa miongoni mwa wanachama wa kwanza wa OIF wakati ilianzishwa Niamey tarehe 20 Machi, 1970.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Mali imesema: "Tangu kuanza kwa kipindi cha mpito nchini Mali, Burkina Faso, na kisha Niger, OIF ... imeonyesha mapendeleo katika kuweka vikwazo ... na kupuuza uhuru na mamlaka ya kujitawala nchi hizo.
Wizara hiyo imeongeza kuwa, viongozi wa mpito wa nchi hizo tatu za Sahel wameamua kuondoka kwenye kundi hilo kama sehemu ya juhudi za kulinda "maslahi halali" ya nchi zao.