Nigeria yaanza uchunguzi wa NGOs zilizofadhiliwa na USAID zinazodaiwa kuunga mkono ugaidi
Wakaguzi wa Nigeria wameanzisha uchunguzi kuhusu shughuli za zaidi ya mashirika kumi yasiyo ya kiserikali, NGO, huku kukiwa na madai kwamba fedha za shirika la misaada la serikali ya Marekani, USAID, zilitumika kufadhili ugaidi nchini Nigeria.
Baraza la Wawakilishi – baraza la chini la bunge la Nigeria – lilitangaza hatua hiyo katika barua iliyoandikwa tarehe 10 Machi, ikiomba mashirika hayo kutoa taarifa za kifedha kuanzia mwaka 2015 hadi 2024.
Kamati ya baraza hilo imesema uchunguzi wa NGOs, ikiwa ni pamoja na Transparency International Nigeria na Global Rights, ambazo zinajihusisha na kazi za haki za binadamu, unalenga “kufichua utambulisho wao halisi, vyanzo vya ufadhili na matumizi yao ya fedha.”
Kamati hiyo imesema uchunguzi huo ni jibu kwa kauli ya mbunge wa Marekani, Scott Perry, ambaye alidai mwezi uliopita kwamba shirika kuu la misaada la serikali ya Marekani, USAID, lilikuwa limepeleka fedha kwa makundi kadhaa ya kigaidi, ikiwa ni pamoja na Boko Haram nchini Nigeria.
Nchi hii yenye watu wengi zaidi barani Afrika imekuwa kitovu cha ugaidi kwa miaka mingi, huku kundi la kigaidi la Boko Haram likifanya mashambulizi mara kwa mara hasa katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Kundi hilo lilianzisha uasi wa silaha mwaka 2009 likidai kuwa linapinga 'elimu ya magharibi' ambapo hadi sasa limeua maelfu ya raia na kupelekea mamilioni kukimbia makazi yao.
Msemaji wa Baraza la Wawakilishi la Nigeria, Akin Rotimi, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba kauli za mbunge wa Marekani zilikuwa “nzito sana kupuuzilia mbali."
Madola ya Magharibi yamekuwa yakidaiwa kuwa yanachochea kwa njia isiyo ya moja kwa moja makundi ya kigaidi barani Afrika ili yaweze kutuma majeshi yao katika nchi hizo kwa lengo la kupora utajiri katika nchi za bara hilo.