Jeshi la Somalia laua magaidi 82 wa al-Shabaab
Jeshi la Anga la Somalia kwa ushirikiano na Shirika la Taifa la Usalama (NISA) limeangamiza magaidi 82 wa kundi la al-Shabaab katika mashambulizi ya anga katika eneo la Lower Shabelle.
Katika taarifa leo Ijumaa, NISA imesema mashambulizi hayo sita ya anga yalifanyika katika maeneo ya Sabiid na Canoole ya Lower Shabelle.
Taarifa hiyo imesema: “Operesheni hizi za kuondoa wapiganaji zilifanyika baada ya Shirika la Taifa la Usalama kupata taarifa kuhusu kundi la Khawarij ambalo lilijaribu kuvuruga usalama katika maeneo ya Sabiid na Canoole."
Khawarij ni neno ambalo serikali ya Somalia hutumia ikimaanisha magaidi wa al-Shabaab.
Shirika hilo la usalama wa taifa pia limetoa wito kwa raia “kuepuka maeneo wanakojificha magaidi ambayo hulengwa na Jeshi la Kitaifa.”
Operesheni hii inakuja baada ya al-Shabaab kuanzisha mashambulizi ya alfajiri dhidi ya wanajeshi wa Somalia walioko katika kijiji cha Sabiid, kilichoko pembezoni mwa mji wa kilimo wa Afgoye.
Afgoye iko kilomita umbali wa 30 (maili 18.6) kusini-magharibi mwa mji mkuu, Mogadishu. Opersheni hiyo dhidi ya Al Shabab imejiri pia siku kadhaa baada ya kundi hilo kujaribu kumuua Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia, alipokuwa akilekea katika uwanja wa ndege jijini Mogadishu.
Somalia imekuwa na matatizo ya usalama kwa miaka mingi, huku vitisho vikuu vikijitokeza kutoka kwa makundi ya kigaidi ya al-Shabaab na ISIS au Daesh.
Tangu mwaka 2007, al-Shabaab imekuwa ikiendelea na mapambano dhidi ya serikali ya Somalia na askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika.
Kundi hilo la kigaidi limeongeza mashambulizi tangu Rais Sheikh Mohamud kutangaza “vita kamili” dhidi yake baada ya kuchaguliwa tena mwaka 2022.