Jeshi la Sudan ladhibiti Ikulu ya Rais mjini Khartoum
Vikosi vya Jeshi la Sudan vimedhibiti Ikulu ya Rais wa nchi hiyo mjini Khartoum leo Ijumaa na hivi sasa linawaandamana wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) ndani ya Suuq al Arabi katikati mwa Khartoum.
Chanzo kimoja cha jeshi la Sudan kimeeleza kuwa awali jeshi hilo lilidhibiti lango la mashariki mwa Ikulu ya Rais na kuua makumi ya askari wa Rapid Support Forces waliokuwa ndani ya ikulu, huku wengine wakifanikiwa kutorokea Suuq al Arabi na Mtaa wa Al-Ghaba katikati mwa Khartoum.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Sudan imesema "Tumewaangamiza wanamgambo wa kigaidi wa Dagalo katikati mwa jiji la Khartoum, Suuq al Arabi, Ikulu ya Rais na wizara za serikali."
Msemaji wa Jeshi la Sudan, Brigedia Jenerali Nabil Abdullah ameongeza kuwa, vikosi vya jeshi vimeua askari na kuharibu zana za adui na kukamata kiasi kikubwa cha vifaa na silaha zao, akisisitiza kwamba "wataendeleza mapambano katika nyanja zote za vita hadi ushindi utakapokamilika na nchi yote isafishwe."
Kwa upande wake, kamanda wa operesheni za jeshi la Sudan mjini Khartoum, Meja Jenerali Mohamed Abdel Rahman Al-Bilawi, ameiambia Al Jazeera kwamba "vikosi vya jeshi vitasonga mbele kuelekea Uwanja wa Ndege wa Khartoum ili kuukomboa na kuwatimua waasi maeneo ya mashariki mwa mji mkuu."
Habai zinasema wapiganaji wa Rapid Support Forces wamejibu mashambulizi hayo kwa kushambulia Ikulu ya Rais kwa kutumia ndege zisizo na rubani, na kuua na kujeruhi idadi kubwa ya watu.
RSF imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba mapambano ya Ikulu ya Rais bado hayajaisha, na kwamba wapiganaji wake bado wako karibu na eneo hilo, wakipigana kwa ushujaa na wale iliyowataja kuwa wanachama wa ISIS, akiashiria jeshi la Sudan na vikundi vya kujitolea vinavyoliunga mkono.