Kesi za Ebola DRC zapanda na kuvuka 1,500, vifo vyafikia 473
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139670-kesi_za_ebola_drc_zapanda_na_kuvuka_1_500_vifo_vyafikia_473
Idadi ya kesi zilizothibitishwa za ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imevuka 1,500 siku ya Ijumaa, baada ya maambukizi mapya zaidi ya 40 kuripotiwa, kulingana na takwimu rasmi, huku juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo na ufuatiliaji zikiendelea.
(last modified 2026-07-06T03:22:18+00:00 )
Jul 06, 2026 03:20 UTC
  • Kesi za Ebola DRC zapanda na kuvuka 1,500, vifo vyafikia 473

Idadi ya kesi zilizothibitishwa za ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imevuka 1,500 siku ya Ijumaa, baada ya maambukizi mapya zaidi ya 40 kuripotiwa, kulingana na takwimu rasmi, huku juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo na ufuatiliaji zikiendelea.

Idadi ya vifo nayo imepanda na kufikia 473 tangu mlipuko huo utangazwe rasmi tarehe 15 Mei, kwa mujibu wa taarifa ya hali ya sasa iliyotolewa na Wizara ya Afya Jumamosi.

Mlipuko huu ungali umekita mizizi katika maeneo 34 ya afya katika mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini, na Kivu Kusini, huku zaidi ya watu 11,000 waliokuwa na mawasiliano na wagonjwa wakiwa chini ya uangalizi.

Mamlaka za afya zimeripoti kuwa wagonjwa 213 wamepona, huku wagonjwa 628 wakiendelea kupata matibabu.

Wizara hiyo imesema kuwa uwezo wa uhamasishaji wa jamii unaendelea kuimarishwa ili kukabiliana na upinzani kutoka kwa baadhi ya wananchi, hasa katika eneo la Ituri.

Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) mapema wiki hii viliketi katika mkutano wa ngazi ya juu jijini Kinshasa, ili kuoanisha uongozi wa kisiasa, wadau, na rasilimali kuelekea kipaumbele kimoja: kuisaidia Kongo kwa haraka na kuilinda kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza katika kongamano hilo, Rais Felix Tshisekedi wa DRC alisisitiza umuhimu wa mshikamano na kuimarisha uwezo wa afya wa bara la Afrika kwa ajili ya majibu madhubuti dhidi ya magonjwa ya mlipuko.

Wafadhili na washirika wameahidi kutoa dola milioni 910 kusaidia mapambano dhidi ya Ebola nchini Kongo na Uganda, ambako kesi 20 zimeripotiwa, kulingana na takwimu za Africa CDC.

Tarehe 17 Mei, siku mbili baada ya mlipuko huo kutangazwa nchini Kongo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko wa Ebola unaosababishwa na kirusi cha Bundibugyo, ambao ulienea hadi Uganda, kuwa ni dharura ya afya ya umma inayohitaji tahadhari ya kimataifa.