Licha ya hali mbaya ya kiusalama Somalia, lakini Wasudan wakimbilia nchini humo
Licha ya kwamba usalama nchini Somalia ni mdogo kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya genge la kigaidi la al Shabab, lakini hatari nchini Sudan ni kubwa zaidi kiasi kwamba, wananchi wa Sudan wanaamua kukimbilia Somalia kuokoa maisha yao.
Shirika la habari la Associated Press limeandika makala kuhusu suala hilo na kuandika: Msomi wa Kisudan, Ishag Ali Mohamed amelazimika kuacha kila kitu nyumbani kwake Sudan na kutafuta makazi mapya nchini Somalia na hivi sasa anajisikia yuko nyumbani kabisa licha ya hatari za kiusalama zilizoko Somalia. Msomi huyo mwenye shahada ya PhD anaishi Mogadishu ambako anafundisha Kiarabu kama lugha ya pili katika Chuo cha Media Digital Media Academy.
Mhadhiri Mohamed ameungana na jamii kubwa ya Wasudani wanaoishi mjini Mogadishu wakati huu wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani na anasema, amepata hisia za kipekee, anajiona yuko nyumbani kabisa kwani wanajamii wanakusanyika ili kufuturu pamoja wakishirikiana katika vyakula vya kitamaduni kama vile aseeda na balila na kufanya kwa pamoja ibada za mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kila Ramadhani, jamii ya Wasudan mjini Mogadishu huandaa mashindano ya soka ya wachezaji watano kila upande, ambayo yanajumuisha pia wachezaji wa Somalia. "Kama unavyoona nyuma yangu, mapenzi yametuleta pamoja," Mohamed alisema akiwa anaangalia moja ya mashindano hayo.
"Hivi ndivyo tunavyofanya Ramadhani nzima, mwezi uliojaa pirika nyingi nzuri. Mtu unahisi uko nyumbani, huko katika nchi ya kigeni." Lakini jitihada za Mhadhiri Mohamed kuelekea kwenye usalama wake na familia yake huko Somalia hazikuwa rahisi.
Anaelezea sehemu ya majanga yaliyomkumba akisema: "Moja ya matukio yaliloniumiza sana ni wakati nikiwa nyumbani na familia yangu. Mara kombora kubwa lilianguka kwenye nyumba yetu Liliharibu ukuta, likakata miti na kuvunja milango. Kitongoji kizima kilifikiri kuwa tumekufa."
Vita vya Sudan vimepelekea zaidi ya watu milioni 14 kukimbia makwao.