Balozi wa A/Kusini arejea nyumbani kutoka US kwa ufakhari mkubwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124312-balozi_wa_a_kusini_arejea_nyumbani_kutoka_us_kwa_ufakhari_mkubwa
Balozi wa Afrika Kusini ambaye rais wa Marekani Donald Trump ametaka aondoke nchini humo kutokana na kukosoa sera zake, amerejea Afrika Kusini kwa ufakhari mkubwa na kupokewa kwa shangwe.
(last modified 2025-03-24T07:23:06+00:00 )
Mar 24, 2025 07:23 UTC
  • Balozi wa A/Kusini arejea nyumbani kutoka US kwa ufakhari mkubwa

Balozi wa Afrika Kusini ambaye rais wa Marekani Donald Trump ametaka aondoke nchini humo kutokana na kukosoa sera zake, amerejea Afrika Kusini kwa ufakhari mkubwa na kupokewa kwa shangwe.

Balozi Ebrahim Rasool na mkewe, Rosieda, waliwasili jana katika Uwanda wa Ndege wa Kimataifa wa Cape Town baada ya kusafari kwa muda wa saa 32 kutoka Marekani kupitia Qatar na wamekaribishwa vyema na kwa shangwe na mamia ya wafuasi wao.

Mapema mwezi huu, Balozi Rasool alitangazwa na serikali ya Marekani kuwa ni mtu asiyetakiwa kuweko nchini humo baada ya kukosoa sera za Donald Trump, hatua ambayo inaonesha wazi jinsi madai ya uhuru wa kusema yasivyothaminiwa nchini Marekani licha ya majigambo makubwa ya Washington ya kupigania haki za binadamu na demokrasia. 

Akiwahutubia mamia ya mashabiki wake kwenye uwanja wa ndege wa Cape Town, Balozi Rasool amesema kwamba ingawa ametakiwa kuondoka huko Marekani lakini jambo hilo limeshindwa kufikia lengo lake kwani viongozi wa Marekani wanadhani wamemdhalilisha wakati yeye anaona fakhari kwa maneno aliyotoa na wananchi wa Afrika Kusini nao wanajivunia msimamo huo ndio maana wamejitokea kwa mamia kumpokea kishujaa. 

Amesema: "Unaporejea nyumbani na kupokewa kwa shangwe na umati kama huu wa watu, mtu unaona fakhari na unajivunia msimamo wako."

Alipoulizwa iwapo diplomasia imeshindwa, amesema ukweli kwamba matamshi yake yamemfanya Trump na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio kuwa makini na hatua ya serikali ya Marekani ya kumtangaza kuwa ni mtu asiyetakiwa nchini humo ni ushahidi kwamba ujumbe wake umefika ngazi za juu kabisa za serikali ya Marekani.