Angola yajiondoa kama mpatanishi wa mgogoro wa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124326-angola_yajiondoa_kama_mpatanishi_wa_mgogoro_wa_drc
Angola imejiondoa kama mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2025-03-25T02:41:52+00:00 )
Mar 25, 2025 02:41 UTC
  • Angola yajiondoa kama mpatanishi wa mgogoro wa DRC

Angola imejiondoa kama mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ofisi ya rais wa Angola ilitoa tangazo hilo Jumatatu huku kukiwa na hasira baada ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya waasi wa M23 na serikali ya Kinshasa kusambaratika hivi karibuni.

Ofisi ya rais wa Angola imeongeza kuwa jukumu la Rais Joao Lourenco kama mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, ambalo alikabidhiwa mwezi Februari, ndilo litakalokuwa kipaumbele chake katika siku zijazo.

Tangazo hili linakuja baada ya kushindwa jaribio la hivi karibuni la kuandaa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya waasi wa M23 na serikali ya Kongo yaliyopangwa kufanyika Machi 18 katika mji mkuu wa Angola, Luanda. Waasi walitangaza ghafla kujiondoa katika mazungumzo hayo.

Kupitia juhudi zake za upatanishi, Rais Lourenco alifanikiwa kuishawishi serikali ya DRC na waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kuhusika katika mazungumzo ya moja kwa moja.

Mnamo Julai 30, 2024, mkutano wa mawaziri kuhusu hali ya usalama na amani mashariki mwa DRC ulipelekea kusitishwa mapigano katika mji mkuu wa Angola, Luanda kuanzia Agosti 4 ya mwaka huo.

Wiki iliyopita, Rais Felix Tshisekedi wa Kongo na Rais Paul Kagame wa Rwanda walifanya mazungumzo ya ghafla huko Doha, Qatar. Huo ulikuwa mkutano wa kwanza kati ya viongozi hao tangu M23 ilipoteka miji mikuu ya mikoa ya Goma na Bukavu mwaka huu.

Mazungumzo hayo yalifanyika chini ya upatanishi wa Amiri wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani.

Wakati huo huo, Rwanda imekaribisha uamuzi wa waasi wa M23 wa kujiondoa kutoka mji wa kimkakati wa madini wa Walikale.

Taarifa kutoka ofisi ya msemaji wa serikali imesema Rwanda inaunga mkono mipango ya kuelekea makubaliano ya kudumu ya kisiasa na kiusalama ili kumaliza vita katika eneo hilo.

Kulingana na taarifa ya UN iliyotolewa Ijumaa, katika kipindi cha chini ya miezi mitatu, idadi ya raia wa DRC walioakimbia mgogoro kuelekea nchi jirani imeongezeka hadi zaidi ya watu 100,000,