Somalia yajiunga na Afreximbank ili kukuza biashara ya ndani ya Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124334-somalia_yajiunga_na_afreximbank_ili_kukuza_biashara_ya_ndani_ya_afrika
Kuanzia jana Jumatatu, Somalia imekuwa rasmi mwanachama wa 53 wa Benki ya Mauzo ya Nje ya Afrika (Afreximbank) wakati huu ambapo nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika imo kwenye jitihada za kukuza biashara ya ndani ya Afrika na uchumi wake.
(last modified 2025-03-25T03:14:20+00:00 )
Mar 25, 2025 03:14 UTC
  • Somalia yajiunga na Afreximbank ili kukuza biashara ya ndani ya Afrika

Kuanzia jana Jumatatu, Somalia imekuwa rasmi mwanachama wa 53 wa Benki ya Mauzo ya Nje ya Afrika (Afreximbank) wakati huu ambapo nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika imo kwenye jitihada za kukuza biashara ya ndani ya Afrika na uchumi wake.

Taasisi hiyo ya fedha ya kimataifa ya barani Afrika imesema kwenye taarifa yake kwamba Somalia imekubaliwa rasmi kuwa mwanachama wa benki hiyo ili kuwezesha upatikanaji wa rasilimali za kifedha na fursa za uwekezaji zinazolenga kuimarisha miundombinu, kustawisha biashara na kujenga uwezo wake wa kiuchumi.

Hirsi Jama Ganni, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Somalia anayehusika na mambo ya nje amesema kuwa, makubaliano hayo muhimu yanaashiria dhamira yao ya kuwa wahusika wakuu katika maendeleo ya kikanda na ya bara zima, hasa kupitia biashara inayoendeshwa chini ya mfumo wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.

Waziri Jama amesema: "Ushirikiano huu ni muhimu kwa ajili ya juhudi zinazoendelea za ujenzi mpya uchumi wa Somalia na kufungua milango ya kufikishiwa Somalia misaada ya kifedha na kiufundi."

Kwa upande wake, Benedict Oramah, mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Afreximbank amesema: "Tuna furaha kuikaribisha Somalia katika familia ya Afreximbank. Hii ni hatua muhimu kwani itapanua fursa za sekta za umma na binafsi za Somalia na kuiwezesha kupata ufadhili na afua nyingine ambazo zitashughulikia mahitaji halisi ya Wasomali."

Afreximbank imeongeza kuwa, imeanzisha majadiliano na sekta ya biashara na fedha ya Somalia kwa ajili ya kuisaidia kukuza uchumi wake wa ndani ya nchi.