Tanzania yaripoti kupungua kwa asilimia 40 maambukizi mapya ya TB
Tanzania imeungana na jumuiya ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani (TB) ikisema kuwa, serikali imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya Kifua Kikuu kwa takriban asilimia 40 katika kipindi cha miaka minane.
Katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku hiyo ambayo huwa inaadhimishwa kimataifa Machi 24 kila mwaka ili kuongeza kasi ya kukomesha ugonjwa wa Kifua Kikuu, Naibu Waziri wa Afya wa Tanzania, Godwin Mollel amesema kuwa, maambukizi mapya ya Kifua Kikuu yalipungua kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mwaka 2015 hadi wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000 mwaka 2023.
Mollel amesema katika taarifa yake iliyotolewa Ikulu ya Dodoma kuwa vifo vinavyotokana na TB vimepungua nchini Tanzania kutoka 56,000 mwaka 2015 hadi 18,400 mwaka 2023, upunguaji ambao ni takriban asilimia 67.
Ameongeza kuwa, juhudi hizo zimeifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 13 duniani zinazofanya vizuri katika jitihada za kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa wa TB kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2025 kama yanavyosema makadirio ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Amesema mafanikio ya kupambana na TB Tanzania yanatokana na juhudi za serikali za kuboresha vifaa vya uchunguzi na dawa maalumu kwa ugonjwa huo.
Kauli mbiu ya kampeni ya mwaka huu Tanzania ni: "Ndiyo! Tunaweza Kukomesha Kifua Kikuu: Jitume, Wekeza, Toa."
WHO inapendekeza kwamba serikali za dunia ziwekeze katika kuimarisha mifumo yao ya afya ili kuboresha upatikanaji wa huduma za kutibu TB, hasa katika maeneo ya vijijini na kuweka kipaumbele katika kuongeza uchunguzi, utambuzi, matibabu, msaada wa kisaikolojia na lishe kwa kuzingatia idadi ya watu waliooko hatarini.