Rwanda yapinga kauli ya rais wa Burundi kwamba inapanga kushambulia nchi yake
Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda amesema kwamba kauli ya Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, kwamba Rwanda inapanga kushambulia nchi yake ni "ya kusikitisha."
Olivier Nduhungirehe ameandika kwenye ukurasa wa kijamii wa X kwamba maafisa wa kijeshi na usalama wa nchi hizo mbili wamekuwa katika majadiliano na hata kukubaliana kuhusu umuhimu wa kupunguza mivutano.
Amesema alijadili suala hili na mwenzake wa Burundi katika mkutano wa pamoja wa mawaziri wiki iliyopita kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare, na kwamba walikuwa "katika mawazo sawa kabisa" .
Nduhungirehe amesema Rwanda itaendelea kujitolea kwa ajili ya amani na Burundi na katika eneo la Maziwa Makuu lakini kwamba inatarajia "utulivu kidogo" katika matamshi rasmi kutoka upande wa pili wa Mto Akanyaru.
Tamko la waziri wa mambo ya nje limekuja baada ya Rais Ndayishimiye kusema katika mahojiano na BBC kwamba Rais Paul Kagame wa Rwanda, anapanga kushambulia Burundi.
"Warundi hawatakubali kuuawa kama Wakongo wanavyouawa. Watu wa Burundi ni wapiganaji," alisema Ndayishimiye, akiongeza kuwa Burundi haina mpango wa kushambulia Rwanda na kuwa inataka kutatua tatizo hilo kupitia mazungumzo.
Amesema pia kwamba Rwanda ilikuwa nyuma ya jaribio la mapinduzi la mwaka 2015 nchini Burundi.
Baada ya jaribio hilo la mapinduzi kushindikana, Burundi ilifunga mpaka wake na Rwanda na kuufungua tena baada ya zaidi ya miaka mitano.