Rais Ruto: Mwanasheria Mkuu aliyefutwa kazi alichelewesha tume ya wakfu wa Waislamu
-
Rais William Ruto akiwasili katika dhifa ya Futari katika Ikulu ya Nairobi, 25 Machi 2025
Rais William Ruto wa Kenya amemkosoa hadharini aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, akitaja kipindi chake cha uongozi kuwa "kisichofaa" katika kushughulikia masuala muhimu ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Tume ya Wakfu wa Kiislamu. Kwa muda mrefu uanzishwaji wa mfuko huo umekuwa kilio cha Waislamu wa Kenya.
Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi wakati wa dhifa ya Futari na Waislamu wa matabaka mbali mbali Jumanne, Rais Ruto alimlaumu Muturi kwa kuchelewesha uanzishwaji wa Tume ya Wakfu kwa ajili kusimamia mali za Waislamu.
Rais Ruto akiwahutubu Waislamu amesema: “Ninakubaliana nanyi kwamba Tume ya Wakfu wa Kiislamu umechukua muda mrefu. Hakuna sababu ya kucheleweshwa. Nilikuwa na tatizo na Mwanasheria Mkuu ambaye alikuwa pale, alikuwa na uwezo mdogo, lakini sasa tuna mwanamke mwenye uwezo na naweza kukuhakikishia kwamba suala hili litatatuliwa."
Tume hiyo inatazamiwa usimamia mapato yanayotokana na mali za wakfu. Mapato hayo yanapaswa kutumika kusaidia malengo ya hisani kama elimu, huduma za afya, na huduma za kijamii.
Punde baada ya kauli ya Ruto, Justin Muturi, ambaye leo pia amefutwa kazi katika wadhifa aliokuwa nao wa Waziri wa Utumishi wa Umma, amemjibu na kukanusha kuhusika katika kuchelewesha utekelezaji wa Mfuko wa Wakfu akisisitiza kuwa hakuna mfuko kama huo katika sheria.
Muturi, amemjibu Ruto kupitia ukurasa wake wa X , ambapo amedai kuwa Sheria ya Wakfu ya mwaka 2022 haijaafiki uwepo wa mfuko kama huo.
Mbali na suala la Wakfu, Rais Ruto alitumia hafla hiyo ya futari kusisitiza dhamira ya serikali yake ya kujumuisha jamii zote, akiwahakikishia Waislamu kuwa wana nafasi muhimu katika uongozi wa taifa.
Pia ameahidi kutambua rasmi jamii ya Wanubia, ambao ni Waislamu, kama sehemu ya makabila ya Kenya ifikapo Madaraka Dei au Jamhuri Dei mwaka huu.
Aidha, amezungumzia ucheleweshaji wa ujumuishaji wa elimu ya Kiislamu katika mtaala wa taifa, na ameahidi kushughulikia changamoto hiyo mara moja.