UN yasikitishwa na kuendelea mashambulizi dhidi ya raia nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124398-un_yasikitishwa_na_kuendelea_mashambulizi_dhidi_ya_raia_nchini_sudan
Msemaji Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kuendelea mashambulizi dhidi ya raia nchini Sudan, ikiwa ni pamoja na shambulio baya la anga lililofanywa kwenye soko la Darfur Kaskazini, kumeutia wasiwasi mkubwa umoja huo.
(last modified 2025-03-26T22:50:14+00:00 )
Mar 26, 2025 22:50 UTC
  • UN yasikitishwa na kuendelea mashambulizi dhidi ya raia nchini Sudan

Msemaji Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kuendelea mashambulizi dhidi ya raia nchini Sudan, ikiwa ni pamoja na shambulio baya la anga lililofanywa kwenye soko la Darfur Kaskazini, kumeutia wasiwasi mkubwa umoja huo.

Stephane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema hayo na kuongeza kuwa, umoja huo una wasiwasi mkubwa pia kuhusu kuongezeka mashambulizi kwenye maeneo yenye watu wengi mjini Khartoum. Matamshi hayo yamekuja baada ya shambulizi la Jumatatu usiku lililotokea Darfur Kaskazini ambalo lilijeruhi watu kadhaa baada ya kupiga soko lililoko umbali wa takriban kilomita 40 kaskazini magharibi mwa mji wa El Fasher.

Dujarric pia amesema kwamba, siku ya Jumapili, kulikuwa na ripoti za raia waliouawa na kujeruhiwa wakati mizinga ilipopiga Msikiti mmoja mashariki mwa Khartoum wakati Waislamu wakiwa kwenye Sala ya jamaa. Raia wengi pia wameripotiwa kujeruhiwa katika mashambulizi makali ya risasi yaliyotokea Omdurman mji unaopakana na Khartoum.

Sehemu moja ya matamshi ya Dujarric imesema: "Umoja wa Mataifa unazikumbusha pande zote katika mzozo wa Sudan kuwa zina wajibu wa kuchunga majukumu yao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kulinda usalama wa raia na miundombinu ya kiraia, na kuchukua hatua zote zinazowezekana za kuepuka kuwasababishia madhara raia."

Msemaji huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amesema kuwa, vita visivyoisha vinaendelea kuwasababishia hasara kubwa raia na vimevuruga mno mfumo wa huduma za afya nchini Sudan, ikiwa ni pamoja na katika eneo la Darfur. Mwezi uliopita pekee, karibu nusu ya mashambulizi yayoliripotiwa kupiga vituo vya afya nchini Sudan, yalitokea Darfur.