Umoja wa Afrika wataka kufadhiliwa zaidi juhudi za amani nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124400-umoja_wa_afrika_wataka_kufadhiliwa_zaidi_juhudi_za_amani_nchini_somalia
Mwenyekiti mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika AU, Mahmoud Ali Youssouf, ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuongeza misaada yao ya kufanikisha juhudi za kuleta utulivu nchini Somalia.
(last modified 2025-03-26T22:50:54+00:00 )
Mar 26, 2025 22:50 UTC
  • Umoja wa Afrika wataka kufadhiliwa zaidi juhudi za amani nchini Somalia

Mwenyekiti mpya wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika AU, Mahmoud Ali Youssouf, ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kuongeza misaada yao ya kufanikisha juhudi za kuleta utulivu nchini Somalia.

Youssouf, ambaye amemaliza ziara yake ya kwanza nchini Somalia tangu achaguliwe kuwa Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, amegusia upungufu mkubwa wa fedha unaokwamisha juhudi za AU za kurejesha utulivu na amani nchini Somalia na kutoa mwito wa kuongezwa ufadhili na misaada ya kimataifa ya kufanikisha jukumu hilo zito lakini muhimu mno.

Amesema: "Tayari nimeanza kazi hapa Addis Ababa ya kuzungumza na baadhi ya washirika wetu ili Somalia isitelekezwe wala kuachwa peke yake. Somalia itaendelea kuwa kitovu cha ushirikiano wa jamii ya kimataifa." Ameahidi kushirikiana na washirika wa kimataifa wa Somalia na kusisitizia umuhimu wa kuweko msaada endelevu kwa Somalia katika vita vyake na genge la kigaidi la al-Shabaab.

 

Katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, Youssouf amesema kuwa, ujumbe wa amani wa AU nchini Somalia ATMIS uko kwenye kipindi cha mpito. Amesema: "Ninataka kusisitiza hapa kwamba tunao uwezo wa kuzishinda changamoto hizi. Lakini tunahitaji kujitolea, tunahitaji ushirikiano na tunahitaji kuungwa mkono na jamii ya kimataifa." 

Kwa upande wake, Rais wa Somalia ameonesha matumaini yake ya kuweza AU kuzishinda changamoto zinazoukabili ujumbe wa amani wa umoja huo kupitia ushirikiano na uongozi mpya wa Kamisheni ya AU. Amesema: "Inonekana kuwa changamoto zilizopo zitatauliwa hasa kwa kuzingatia uzoefu na majaribio yenye mafanikio makubwa ya jitihada za AU za kutafuta amani barani Afrika.