Sudan Kusini yasema Naibu Rais Machar alikamatwa akijaribu kuchochea uasi
Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kwamba Naibu Rais wa Kwanza, Riek Machar, amekamatwa na atachunguzwa kwa tuhuma za kujaribu kuchochea uasi.
Serikali ya Sudan Kusini Ijumaa imethibitisha rasmi kwa mara ya kwanza kukamatwa kwake, jambo ambalo limeibua wasiwasi kuwa linaweza kuanzisha tena vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ripoti kwamba Machar - mpinzani wa muda mrefu wa Rais Salva Kiir - alikamatwa Jumatano zilisababisha wito wa kimataifa kuchukuliwa hatua za kupunguza taharuki. Nchi jirani ya Kenya imemtuma waziri mkuu wake wa zamani, Raila Odinga, kusaidia kupunguza mvutano.
Chama cha Machar kimesema wiki hii kwamba kukamatwa kwake kimsingi kumebatilisha makubaliano ya amani ya mwaka 2018 ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano kati ya wapiganaji wa kabila la Dinka wanamfuata Kiir na wapiganaji wa kabila la Nuer wanaomfuata Machar.
Msemaji wa serikali na waziri wa habari Michael Makuei amesema katika taarifa kwamba "Machar na wenzake wanaopinga amani katika chama cha SPLM/A-IO (chama cha Machar), wamekamatwa na watachunguzwa na kuletwa mbele ya vyombo vya sheria."
Alimshutumu Machar kwa kuwasiliana na wafuasi wake na "kuwasukuma kuasi dhidi ya Serikali kwa lengo la kuharibu amani ili uchaguzi usifanyike na Sudan Kusini irejee vitani."
Aidha amesema:"Makubaliano ya Amani hayajavunjika na hayatavunjika chini ya hali yoyote."
Hakukuwa na jibu la haraka kutoka kwa Machar au chama chake kuhusu tuhuma hizo. Hayo yanajiri baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres kusema anasikitishwa sana na kuendelea kushtadi taharuki na hali ya mambo nchini Sudan Kusini.
Kupitia msemaji wake, Stephane Dujarric, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba, nchi hiyo ya Kiafrika ipo katika ncha ya kutumbukia tena kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) umetoa wito kwa pande zote nchini humo "kujizuia na kuzingatia Mkataba Uliohuishwa wa Amani (RPA)."