Al Burhan apinga mazungumzo Sudan, atangaza ushindi kamili
Abdel Fattah Al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Mpito la Sudan ambaye pia ni Mkuu wa Jeshi la Sudan SAF, amepinga vikali mazungumzo ya aina yoyote ile na wapiganaji wa Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF na kutangaza ushindi kamili dhidi ya vikosi hivyo.
Katika hatua ambayo inahesabiwa ni pigo kubwa kwa RSF, tarehe 21 jeshi la Sudan lilitangaza kuwa limeteka ikulu ya rais na majengo muhimu ya serikali katikati mwa Khartoum mji mkuu wa Sudan. Siku tano baadaye, jeshi lilidai kuudhibiti Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum, ambao ulikuwa ukishikiliwa na RSF tangu mwezi Aprili 2023.
Al-Burhan amesema: "Hakutakuwa na mazungumzo wala maelewano na RSF. Ninatilia mkazo ahadi ya jeshi kwa wananchi kwamba hakutakuwa na kurudi nyuma hadi tutakapowashinda na kuwaangamiza wanamgambo."
Maafisa wa kijeshi wa Sudan walisema wiki iliyopita kwamba jeshi la SAF sasa linadhibiti eneo lote la Khartoum, mojawapo ya majimbo matatu makuu ya utawala nchini humo.
Mgogoro wa takriban miaka miwili kati ya SAF na RSF umesababisha makumi ya maelfu ya watu kuuawa, kuwa wakimbizi zaidi ya watu milioni 15, na kuisukuma Sudan kwenye ukingo wa janga la njaa. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa.
Vita hivyo vimeporomosha kabisa mfumo wa huduma ya afya nchini Sudan huku takwimu za majeruhi zikiendelea kuwa ngumu kujulikanana kutokana na mazingira mabaya na tata ya vita.
Juhudi za kupatanisha na kuleta usitishaji mapigano zimekwama, huku pande zote mbili zikishutumiwa kukiuka haki za binadamu na kuzuia misaada ya kibinadamu.