Gabon yaanza kampeni ya urais kabla ya uchaguzi wa Aprili 12
Kampeni za uchaguzi wa urais nchini Gabon zimeanza rasmi siku ya Jumamosi na zitaendelea hadi Aprili 11. Upigaji kura utafanyika Aprili 12.
Rais wa Mpito, Brice Clotaire Oligui Nguema, aliyeongoza mapinduzi ya Agosti 2023 na baadaye kujiuzulu kutoka jeshini ili kugombea urais, ametoa wito kwa wapiga kura kumuunga mkono, akibainisha kuwa sheria ya uchaguzi ya Gabon inaruhusu wanajeshi kugombea baada ya kuomba likizo rasmi.
Katiba ya Gabon inaweka muhula wa miaka saba kwa urais, ambao unaweza kurejewa mara moja tu. Aidha, ina vifungu vinavyokataza urithi wa madaraka ndani ya familia, kwa kuzuia wake au watoto wa rais aliyeshahudumu mihula miwili kugombea nafasi hiyo.
Wagombea wanane, akiwemo Nguema, wanachuana kuwania urais. Mpinzani mkuu wa Nguema anatarajiwa kuwa Alain Claude Billie By Nze, waziri mkuu wa zamani wa Gabon, anayegombea kama mgombea huru.
Wagombea wengine waliopitishwa ni pamoja na Stephane Germain Iloko Boussengui, aliyekuwa mwanachama wa chama cha rais wa zamani Omar Bongo na sasa anaongoza harakati yake mwenyewe iitwayo “mkusanyiko wa upinde wa mvua mkubwa”, pamoja na Joseph Lapensee Essigone, mkaguzi wa kodi.
Iwapo hakuna mgombea atakayepata kura nyingi zaidi ya nusu tarehe 12 Aprili, Mahakama ya Katiba itapanga duru ya pili ya uchaguzi.