Lubanga, mbabe wa kivita aunda kundi jipya la waasi DRC
Aliyekuwa kinara wa genge moja la waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Thomas Lubanga na ambaye alikuwa mtu wa kwanza kukamatwa na kufungwa jela na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), amezindua kundi jipya la waasi nchini humo.
Hatua ya Lubanga ya kuzindua harakati ya waasi ya Convention for the Popular Revolution (CPR) inakuja wakati huu ambapo waasi wa M23 wanaendeleza mashambulizi makubwa huko mashariki mwa Kongo DR tangu mwanzoni mwa huu wa 2025, na kudhibiti maeneo na miji mengi, ikiwa ni pamoja na Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, na Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.
Lubanga ambaye alikuwa kiongozi wa wanamgambo wa Union of Congolese Patriots-UPC aliwaongoza wanamgambo wa kabila la Hema kupigana dhidi ya watu wa kabila la Lendu.
Ghasia za kugombea ardhi ziligeuka kuwa vita vya kikabila ambapo takriban watu 50,000 waliuawa na maelfu walibaki bila makazi.
Lubanga alipatikana na hatia ya makosa ya ukiukaji wa haki za binadamu kama mauaji na ubakaji wa raia na kuwatumia watoto wakati akiongoza kundi la waasi la UPC kati ya mwaka 1997 hadi 2007 katika jimbo la Ituri.

Ikumbukwe kuwa, mnamo Machi mwaka 2020, ICC ilimuachilia huru Lubanga baada ya kumaliza kifungo chake cha miaka 14. Baada ya kuachiwa huru, Rais Felix Tshisekedi alimteua katika jopokazi la kuleta amani katika mji alikozaliwa mbabe huyo wa kivita, wa Ituri, mashariki mwa DRC.
Mwezi Disemba mwaka 2015, alihamishwa kutoka gereza ya ICC na kupelekwa katika gereza la Makala mjini Kinshasa kumaliza kifungo chake akiwa pamoja na mbabe mwingine wa kivita, Germain Katanga ambaye pia ICC ilimpata na hatia.