Jeshi la Sudan laendelea kupata mafanikio El Fasher, mapigano yanaendelea El Obeid
Vyanzo vya kijeshi vya Sudan vimetangaza kwamba jeshi la nchi hiyo linapiga hatua mpya kusini mwa El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, na kwamba wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) wameshambulia sehemu ya magharibi ya mji huo kwa mizinga.
Awali jeshi la Sudan lilikuwa limetanaza kwamba, limeshambulia maeneo ya RSF kwa silaha nzito kusini mashariki mwa El Fasher.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Sudan imeongeza kuwa mashambulizi hayo yamesababisha hasara za binadamu na nyenzo katika safu za kundi hilo la waasi, ikielezea kuwa RSF imefanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya El Fasher, lakini haikutimiza malengo yaliyokusudiiwa.
Wakati huo huo, vyanzo vya ndani vya Sudan vimeripoti kwamba mapigano yanaendelea kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka magharibi mwa Al-Obeid, mji mkuu wa Jimbo la Kordofan Kaskazini, huko katikati mwa Sudan.
Siku chache ziilizopita kamanda wa RSF, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti) alikiri kwa mara ya kwanza kwamba vikosi vyake vimeondoka Khartoum, ambayo imekombolewa kikamilifu na jeshi la Sudan.
Tangu Aprili 2023, jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka vimekuwa katika vita na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 20,000 na kuibua mgogoro mkubwa zaidi wa wakimbizi na njaa, huku takriban Wasudani milioni 15 wakilazimiika kuhama makazi yao.