Afrika Kusini yaonya kuhusu vita vipya vya ushuru vya Trump
Jana Alkhamisi, Afrika Kusini ilionya kuhusu vita vipya vya ushuru vilivyoanzishwa na rais wa Marekani na kuelezea wasiwasi wake kuhusu ushuru uliowekwa na Donald Trump kwa bidhaa za Afrika Kusini na kusema hilo litakuwa na madhara kwa pande zote mbili.
Juzi Jumatano, rais wa Marekani, Donald Trump alitangaza kiwango cha chini cha ushuru cha asilimia 10 duniani kwa bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje na asilimia 30 ya ushuru kwa Afrika Kusini, ambayo adai ni "wahalifu wakubwa zaidi."
Hata hivyo lengo la Trump la kuidhoofisha sarafu ya Afrika Kusini, rand, limefeli hasa kutokana na taarifa kwamba sarafu ya rand ilipanda thamani licha ya hatua hiyo ya Marekani.
Katika taarifa iliyotolewa Alkhamisi asubuhi, Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini imebainisha wasiwasi wake kuhusu ushuru mpya uliowekwa kwa bidhaa za Afrika Kusini ziendazo Marekani.
Taarifa hiyo imesema: ingawa Afrika Kusini bado ina nia ya kuwa na uhusiano wa kibiashara na Marekani, lakini inasema kuwa, madhara ya hatua hiyo ya upande mmoja ya Marekani, itawadhuru pia wananchi wa nchi hiyo.
Uhusiano kati ya Afrika Kusini na Marekani umezidi kuwa mbaya kutokana na msimamo imara wa serikali ya Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini kuhusu kuwaunga mkono wananchi wa Ghaza na kuiburuza mahakamani Israel kutokana na jinai zake za kutisha dhidi ya Wapalestina. Mwezi uliopita, Marekani ilimtaka Balozi wa Afrika Kusini Ebrahim Rasool aondoke nchini humo, hatua ambayo ilitekelezwa kwa ufakhari mkubwa na balozi huyo ambaye alipokewa kwa shangwe nchini Afrika Kusini.