Umoja wa Afrika wapigia debe Akili Mnemba kuleta mabadiliko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124808-umoja_wa_afrika_wapigia_debe_akili_mnemba_kuleta_mabadiliko
Katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Akili Mnemba (Artificial Intelligence-AI-)barani Afrika, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, ametangaza dhamira ya AU kuiweka Afrika kama kinara katika mapinduzi ya kimataifa ya akili mnemba.
(last modified 2025-04-05T22:56:39+00:00 )
Apr 05, 2025 22:56 UTC
  • Umoja wa Afrika wapigia debe Akili Mnemba kuleta mabadiliko

Katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Akili Mnemba (Artificial Intelligence-AI-)barani Afrika, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, ametangaza dhamira ya AU kuiweka Afrika kama kinara katika mapinduzi ya kimataifa ya akili mnemba.

 Alizungumza kwenye jopo la viongozi wa juu lililojumuisha Rais Paul Kagame wa Rwanda, Waziri Kiongozi Musalia Mudavadi kutoka Kenya, Rais Faure Gnassingbé wa Togo, mjasiriamali Strive Masiyiwa, na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Mawasiliano-ITU-, Doreen Bogdan-Martin.

Kwa mujibu wa taarifa amabayo imetolewa na Umoja wa Afrika baada ya kumalizika mkutano huo, Youssouf amesema kuwa Umoja wa Afrika umepitisha Mkakati wa Bara Afrika kuhusu Akili Mnemba kama dira ya kisera kwa maendeleo. Mkakati huu unaelekeza nchi wanachama kuunganisha Akili Mnemba na mipango ya kitaifa ya maendeleo ili kuharakisha ukuaji wa uchumi, uvumbuzi, na mabadiliko ya kidijitali kwa wote.

Kupitia mpango wa utekelezaji wa miaka mitano, AU inasaidia nchi wanachama kutunga sera, kukuza vipaji vya ndani, kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma, na kuhakikisha matumizi ya akili mnemba katika utawala, afya, kilimo na tabianchi. Aidha, juhudi zinafanywa kuendeleza miundombinu ya akili mnemba, kushughulikia changamoto za kisheria na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Youssouf amesisitiza kuwa akili mnemba itakuwa kiini cha uchumi wa kidijitali ndani ya Eneo Huru la Biashara la Afrika. Pia aliangazia umuhimu wa teknolojia hiyo kuakisi lugha na tamaduni za Kiafrika, ili kuhakikisha ushirikishwaji wa kweli wa raia wote katika zama hizi mpya za akili mnemba.

Aidha amesema moja ya vipaumbele vikuu kwa akili mnemba barani Afrika ni kuendeleza suluhisho za akili mnemba zinazowakilisha lugha za Kiafrika na utofauti wa kitamaduni. Hili ni muhimu sana ili kuhakikisha kuwa matumizi ya Akili Mnemba yanajumuisha kila mtu na kuzuia kutengwa kwa kidijitali. Amesisitiza kuwa ubunifu unaoendeshwa na Akili Mnemba lazima uhudumie Waafrika wote, kwa kuwezesha ushiriki sawa katika uchumi wa kidijitali.