Kenya: Suluhisho la kudumu kwa mzozo wa DRC linapaswa kuwa la ndani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124810-kenya_suluhisho_la_kudumu_kwa_mzozo_wa_drc_linapaswa_kuwa_la_ndani
Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya, Moses Wetang'ula, amesema kwamba suluhisho la kudumu kwa mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) linapaswa kuwa la ndani, likizingatia mapendekezo kutoka kwa nchi za eneo.
(last modified 2025-04-05T22:57:40+00:00 )
Apr 05, 2025 22:57 UTC
  • Kenya: Suluhisho la kudumu kwa mzozo wa DRC linapaswa kuwa la ndani

Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya, Moses Wetang'ula, amesema kwamba suluhisho la kudumu kwa mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) linapaswa kuwa la ndani, likizingatia mapendekezo kutoka kwa nchi za eneo.

 Akizungumza Jumamosi jijini Nairobi baada ya kukutana na Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, ambaye ni mmoja wa wawezeshaji watano wa mazungumzo ya kusaka amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Wetang'ula amesisitiza kuwa uzoefu wake unaonyesha kuwa suluhisho zinazoongozwa na Waafrika kwa migogoro ya bara huwa na zina ufanisi zaidi.

Ameongeza kuwa diplomasia ya ndani, inayotegemea uelewa wa kihistoria na dhamira ya pamoja, ni muhimu katika kufungua uwezo kamili wa kanda hiyo.

Wetangula amesema: "Napongeza juhudi za kidiplomasia zinazoendelea na zilizoimarishwa za viongozi wa Afrika. Ni kupitia upatanishi wa kiwango cha juu na nia ya pamoja ya kisiasa ndipo tunaweza kupata amani na maendeleo ya kudumu kwa watu wetu."

Obasanjo anaungana na Rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, na marais wa zamani Kgalema Motlanthe (Afrika Kusini), Sahle-Work Zewde (Ethiopia), na Catherine Samba-Panza (Jamhuri ya Afrika ya Kati) katika jopo la pamoja la kuwezesha mazungumzo kuhusu DRC.

Jopo hili litafanya kazi chini ya mwamvuli wa Umoja wa Afrika, likipata msaada wa moja kwa moja kutoka kwa jumuiya za kanda kama Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.

Wetang'ula amesisitiza kuwa juhudi za awali za amani zilizoshindikana DRC zinaonyesha haja ya suluhisho za ndani kuwa mstari wa mbele. "Kama waziri wa mambo ya nje, nilifanya kazi na marehemu Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa, kuhusu mzozo wa DRC mwaka 2009. Tatizo lile lile bado lipo miaka 14 baadaye," amebainisha Wetang'ula.