Ripoti: Nigeria yapanga mashambulizi dhidi  ya Wafuasi wa Sheikh Zakzaky jijini Abuja
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124866-ripoti_nigeria_yapanga_mashambulizi_dhidi_ya_wafuasi_wa_sheikh_zakzaky_jijini_abuja
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na tovuti ya Sahara Reporters, maafisa wa usalama wa Nigeria wanapanga mashambulizi dhidi ya makazi na mali za wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria (IMN).
(last modified 2025-04-07T03:55:39+00:00 )
Apr 07, 2025 03:55 UTC
  • Ripoti: Nigeria yapanga mashambulizi dhidi  ya Wafuasi wa Sheikh Zakzaky jijini Abuja

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na tovuti ya Sahara Reporters, maafisa wa usalama wa Nigeria wanapanga mashambulizi dhidi ya makazi na mali za wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria (IMN).

Taarifa hiyo, ikinukuu vyanzo vya ndani, inaeleza kuwa oparesheni hiyo inatarajiwa kufanyika siku ya Jumatatu katika maeneo mbalimbali ya jiji la Abuja na viunga vyake.

Ripoti hiyo pia inasema kuwa baadhi ya maafisa wa usalama wamewaonya jamaa zao kuepuka maeneo yanayohusiana na Waislamu wa madhehebu ya Shia katika maeneo hayo, wakihofia uwezekano wa machafuko.

Chanzo kimoja kilidokeza kuwa:“Kuna mpango wa kushambulia makazi na vituo vya wafuasi wa Sheikh Al-Zakzaky siku ya Jumatatu, katika maeneo kama vile Maitama, Asokoro, Garki, Barabara ya Uwanja wa Ndege, na Maraba.”

Mnamo Machi 28, 2025, watu wasiopungua 26 waliripotiwa kuuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa, baada ya Jeshi la Nigeria kuwashambulia wanachama wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria waliokuwa wakifanya maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika mji mkuu, Abuja.

Video kutoka eneo la tukio zinaonyesha vikosi vya usalama vikiwa vimezingira maandamano hayo huku waandamanaji wakikimbia kujificha na  risasi zikisikika zikirindima. Katika video hiyo, wanajeshi wanaonekana wakiburuta mwili wa raia aliyepoteza maisha na kuutupa kwenye gari la kubebea mizigo, huku wakimpiga waandamanaji wengine wawili na kuwalazimisha kuingia kwenye gari jingine la kijeshi.

Ingawa maandamano hayo yalifanyika kwa amani katika maeneo mengine ya Nigeria, maandamano ya Abuja pekee ndiyo yalilengwa na kushambuliwa na vikosi vya jeshi.

Waandamanaji walikuwa wakitembea kwa amani baada ya kuswali Ijumaa katika eneo la Banex Plaza kabla ya kushambuliwa na wanajeshi waliokuwa wamepiga kambi karibu na msikiti huo.

Ofisi ya Mshauri wa Usalama wa Taifa nchini Nigeria ilikuwa imesisitiza kuwa maandamano ya Siku ya Quds yalihitaji kusitishwa “ili kuzuia uvunjifu wa amani” kutoka kwa waandamanaji wanaounga mkono Palestina.

Kwa mujibu wa barua ya ndani iliyovuja, na ambayo imeonwa na Tume ya Haki za Binadamu ya Kiislamu (IHRC), mamlaka za Nigeria zilieleza wasiwasi kuwa licha ya maandamano hayo kuwa ya amani, waandamanaji hao wangeweza kushambulia maslahi ya Marekani na Israel nchini humo, hivyo yakapaswa kuzuiwa.

Mbinu hiyo imekuwa ikitumika na baadhi ya maafisa wa serikali ya Nigeria wanaoiunga mkono Israel katika miaka ya karibuni ili kushinikiza majeshi ya usalama kuwavamia waandamanaji kwa nguvu.

Mnamo mwaka wa 2023, mtu mmoja aliuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya polisi kufyatua risasi dhidi ya maandamano ya Siku ya Quds mjini Abuja.
Na mwaka 2014, vikosi vya usalama vya Nigeria vilifyatua risasi kwenye maandamano mjini Zaria, na kuwaua waandamanaji 34.