Afrika yashuhudia kupungua vifo vya akina mama na watoto wachanga
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124954
Viwango vya vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga barani Afrika vimepungua tangu mwaka 2000, Shirika la Afya Duniani (WHO) limebaini katika ripoti mpya.
(last modified 2025-06-15T08:05:10+00:00 )
Apr 10, 2025 02:55 UTC
  • Afrika yashuhudia kupungua vifo vya akina mama na watoto wachanga

Viwango vya vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga barani Afrika vimepungua tangu mwaka 2000, Shirika la Afya Duniani (WHO) limebaini katika ripoti mpya.

Kati ya mwaka 2000 na 2020, vifo vya akina mama katika ukanda wa Afrika vilipungua kwa asilimia 40, kutoka vifo 727 hadi 442 kwa kila vizazi hai 100,000, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kasi ya kupungua kwa vifo hivyo bado haitoshi kufikia lengo la Maendeleo Endelevu (SDG) la kuwa na vifo chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya asilimia 60 ya nchi za Afrika sasa zinaripoti kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watoto huzaliwa kwa msaada wa wahudumu wa afya wenye ujuzi, ongezeko kutoka asilimia 28 mwaka 2010. Lakini pamoja mafanikio haya, bado kuna mapengo makubwa hasa katika maeneo ya vijijini na yale yaliyoathiriwa na migogoro.

WHO ilisisitiza kuwa: “Vikwazo vikuu vya maendeleo ni pamoja na ukosefu wa fedha za kutosha, udhaifu katika utawala, uhaba wa wafanyakazi wa afya, na misukosuko ya mara kwa mara kama vile milipuko ya magonjwa na migogoro – yote ambayo huvuruga huduma za afya ya mama na mtoto. Katika maeneo dhaifu na yaliyoathirika na migogoro, wanawake na watoto wako kwenye hatari zaidi.”

Ukanda huu bado unachangia asilimia 70 ya vifo vinavyohusiana na ujauzito na kujifungua duniani, huku kukikadiriwa vifo vya akina mama 178,000 na vifo vya watoto wachanga milioni moja kila mwaka barani Afrika.

Shirika hilo limebainisha sababu kadhaa zinazochangia vifo vya akina mama, ikiwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi, maambukizi, shinikizo la juu la damu wakati wa ujauzito, matatizo wakati wa kujifungua, na utoaji mimba usio salama. Vifo vya watoto wachanga kwa kawaida husababishwa na kuzaliwa kabla ya wakati, matatizo ya kujifungua, na maambukizi. Vifo hivi vingi vinaweza kuzuilika iwapo hatua za haraka zitachukuliwa.

WHO imesisitiza haja ya kuongeza kasi ya juhudi za kuboresha afya ya mama na mtoto mchanga barani Afrika.

Dkt. Chikwe Ihekweazu, Kaimu Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema: “Katika maeneo mengi, ujauzito na kujifungua bado ni matukio ya kuhatarisha maisha ... Kila dola inayowekezwa katika afya ya mama na mtoto inaleta faida kubwa: familia zenye afya, jamii imara na ukuaji wa uchumi endelevu."