Wanawake na watoto, wahanga wakuu wa unyanyasaji wa kingono DRC
(last modified Sat, 12 Apr 2025 06:35:52 GMT )
Apr 12, 2025 06:35 UTC
  • Wanawake na watoto, wahanga wakuu wa unyanyasaji wa kingono DRC

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema katika ripoti yake ya karibuni kabisa iliyotolewa jana Ijumaa kwamba, kwa wastani kila baada ya dakika 30 mtoto mmoja alibakwa wakati wa mapigano makali ya Januari na Februari huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Kwa mujibu wa shirika hilo, watoto ni asilimia 35 hadi 45 ya takriban kesi 10,000 za ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia zilizoripotiwa katika miezi ya mapigano makali ya Januari na Februari mwaka huu na ambazo zimewahusu wanawake na watoto wa kike.

Msemaji wa UNICEF James Elder amewaambia waandishi wa habari katika mkutano wa Umoja wa Mataifa huko Geneva Uswisi kwamba: "Wakati wa kipindi kigumu mno ya mgogoro wa vita mwaka huu huko mashariki mwa DRC, tathmini zinaonesha kuwa mtoto mmoja alibakwa kila baada ya nusu saa."

"Hatuzungumzii tukio moja moja bali tunazungumzia mgogoro wa kimfumo. Tunawaona wahanga wakiwa na umri mdogo mno. Ni silaha ya vita na mbinu ya makusudi ya ugaidi. Na inaharibu familia na jamii," Elder amesema.

Taarifa mbalimbali zinasema kuwa, idadi ya vitendo vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake na watoto mashariki mwa DRC ni kubwa na kwa kawaida haviripotiwi kutokana na hofu, unyanyapaa na wasiwasi wa kushambuliwa zaidi na magenge ya wahalifu bila ya kupata mtu wa kuwalinda wahanga hao.

Msemaji wa UNICEF ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na za pamoja za kupambana na ukatili huo mkubwa wa kingono. "Tunahitaji juhudi za ziada za kuzuia, kuwatunza wahanga wa unyanyasaji na kutafuta njia salama kwa ajili ya kuwaokoa mahanga hao. Lazima tuwaoneshe wahanga wa unyanyasaji kwamba ulimwengu uko pamoja nao. Na lazima wahalifu wachukuliwe hatua kali na haki itendeke," amesema.