Polisi Kenya wamjibu Gachagua, wasema: Tutakulinda kama raia wengine
-
Rigathi Gachagua
Idara ya Polisi ya Kenya imemwambia aliyekuwa Naibu Rais wa nchi hiyo, Rigathi Gachagua, kwamba italinda usalama wake kama raia wengine na imemtaka kutoa taarifa kwa polisi kuhusu ratiba na mienendo yake ili kuruhusu maafisa kupanga ulinzi wake ipasavyo.
Ni baada ya naibu rais huyo aliyetimuliwa kutoa madai mazito dhidi ya serikali jana Jumanne, akisema kuna mpango mahususi uliosukwa wa kutaka kumuua.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja amemhakikishia Bw Gachagua kuwa, "Wakenya wote wanastahili ulinzi", na amemshauri kushirikiana na polisi wa viwango vyote iwapo atahitaji ulinzi zaidi na kutoa taarifa mapema kuhusu ratiba na shughuli zake za hadhara ili kuwezesha mipango na uratibu wa kiusalama.
Gachagua jana Jumanne alimwandikia barua Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja akilalamikia hatua ya kuondolewa kwa walinzi wake, jambo analosema limemwacha katika hatari ya kuvamiwa na kushambuliwa na na magenge ya wahalifu.
Gachagua, ambaye aliondolewa madarakani mnamo Oktoba 2024 kupitia mchakato wa Bunge, amedai kuwa maisha yake, familia yake na ya wafuasi wake yako hatarini.
Naibu Rais huyo wa tatu wa Kenya alimtaka Bw Kanja kuwafunguliwa mashtaka kwa watu waliohusika na vurugu dhidi yake, kutoa ulinzi rasmi anapohudhuria mikutano ya hadhara, kukomesha kufuatiliwa kwa siri kwa familia yake kunakofanywa na maafisa wa usalama na makazi na mali yake kulindwa.