Ripoti ya Amnesty: RSF imefanya maangamizi ya kikabila nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139568-ripoti_ya_amnesty_rsf_imefanya_maangamizi_ya_kikabila_nchini_sudan
Kikosi cha Msaada wa Haraka nchini Sudan (RSF) kilitenda uhalifu dhidi ya ubinadamu na maangamizi ya kikabila wakati wa mashambulizi yake katika mji wa El-Fasher kati ya 2024 na 2025.
(last modified 2026-07-02T04:13:23+00:00 )
Jul 02, 2026 03:22 UTC
  • Wanamgambo wa RSF
    Wanamgambo wa RSF

Kikosi cha Msaada wa Haraka nchini Sudan (RSF) kilitenda uhalifu dhidi ya ubinadamu na maangamizi ya kikabila wakati wa mashambulizi yake katika mji wa El-Fasher kati ya 2024 na 2025.

Hayo yamesemwa katika ripoti ya Amnesty International iliyotolewa jana Jumatano.

Ripoti pana ya Amnesty imefichua kuwa RSF "ilifanya uhalifu dhidi ya ubinadamu na maangamizi ya kikabila wakati wa kampeni yake ya kuiteka El Fasher."

Shirika hilo lisilo la kiserikali limewahoji waathiriwa au mashahidi 247 kati ya mapema mwaka 2024 na Oktoba 2025 huko Darfur Kaskazini.

Limesema RSF ilishambulia kwa makusudi vitongoji vya kandokando ya El Fasher ambavyo vilikuwa makazi ya watu wa Zaghawa huko magharibi mwa Darfur.

Ripoti hiyo imedai kwamba ukatili mkubwa na wa kupanga ulifanyika dhidi ya watoto ikiwa ni pamoja na mauaji, utekaji nyara, kuajiriwa kwa kulazimishwa na ubakaji.

"Ni doa kwenye dhamiri ya ubinadamu," amesema mkuu wa Amnesty International, Agnes Callamard katika taarifa iliyotolewa jana.

Ripoti hiyo imesema kwamba wapiganaji wa RSF walichoma nyumba muda mrefu baada ya wakazi kukimbia, "ikiashiria nia ya kundi hilo ya kuyafanya maeneo hayo yasiweze kukaliwa tena," sambamba na "maangamizi ya kikabila."

Taarifa ya Amnesty International imesema: Wakati wa shambulio la mwisho la RSF dhidi ya El-Fasher mnamo Oktoba 2025 "mamia waliuawa, na wengine wengi waliteswa au kukamatwa" wakijaribu kukimbia.

Ripoti hiyo pia imeeleza kuwa ukiukaji huo wa haki za binadamu ulifanyika "mara kwa mara na kwa kiwango kikubwa," na kusema "wale walio katika nyadhifa za mamlaka walijua, au walipaswa kujua kilichokuwa kikitokea, na hawakuchukua hatua za kuzuia au kumwajibisha mtu yeyote."

Shirika hilo lisilo la kiserikali la kimataifa limehimiza kusitishwa mapigano mara moja na kupelekwa kikosi cha kimataifa kuwalinda raia huko Darfur nchini Sudan.

Sudan ilitumbukia katika vita vya kikatili kati ya jeshi la taifa na kundi la RSF tangu Aprili 2023, ambavyo vimeua makumi ya maelfu na kuwalazimisha mamilioni ya watu kukimbia makazi yao.

Pande zote mbili zimeshutumiwa kwa kuhusika na ukatili na ukiukwaji wa haki za binadamu.