Mamia hawajapatikana baada ya boti kuteketea moto, kuzama DRC
Mamia wa watu wangali hawajulikani walipo baada ya boti iliyokuwa na mamia ya abiria kuzama baada ya kuwaka moto katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuua watu zaidi ya 50.
Shirika la habari la Associated Press liliripoti jana Alkhamisi kuwa, operesheni ya uokoaji ilikuwa inaendelea hadi jana hiyo kwa msaada wa timu za Msalaba Mwekundu na mamlaka za mkoa, kufuatia ajali hiyo iliyotokea Jumanne usiku katika Mto Congo.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Usimamizi wa Mto Congo, Competent Loyoko, boti hiyo iliyotengenezwa kwa mbao ilikuwa na abiria wapatao 450, iliwaka moto karibu na mji wa Mbandaka, baada ya kuondoka bandari ya Matankumu kuelekea eneo la Bolomba.
Loyoko ameeleza kuwa, boti hiyo iliteketea kwa moto baada ya abiria mmoja aliyekuwa na jiko la mkaa kuwasha moto kwa lengo la kupika chakula.
Abiria kadhaa hususan wanawake na watoto inadaiwa wamefariki dunia baada ya kuruka majini huku wakiwa hawana uwezo wa kuogelea. Takriban watu 100 walionusurika walihamishiwa katika maeneo ya dharura kwenye jengo lililopo mji wa Mbandaka.

Ajali mbaya za boti hutokea mara kwa mara katika maji ya Kongo hususan kutokana na kuwa vyombo vingi vya majini hupakia watu kupita kiasi. Nchi hiyo ina barabara chache za lami katika eneo lake kubwa lenye misitu, na usafiri mkubwa ni wa majini.
Desemba 2024, watu takriban 38 walifariki baada ya kivuko kilichobeba zaidi ya watu 400 waliokuwa wakisafiri kwenda kusherehekea Krismasi kuzama kwenye mto. Mwezi Oktoba, boti nyingine ilizama katika Ziwa Kivu Mashariki mwa DRC na kuua watu 78 huku wengine wakinusurika.