Uganda inapanga sheria kuruhusu mahakama ya kijeshi kuwahukumu raia
-
Kiiza Besigye
Serikali ya Uganda inakusudia kuanzisha sheria ya kuruhusu mahakama za kijeshi kuwahukumu raia kwa baadhi ya makosa hata baada ya jambo hilo kupigwa marufuku na Mahakama ya Juu.
Wanaharakati wa haki za binadamu na wanasiasa wa upinzani, kwa muda mrefu, wamekuwa wakiituhumu serikali ya Rais Yoweri Museveni kuwa inatumia mahakama za kijeshi kuwafungulia mashitaka viongozi wa upinzani na wafuasi wao kwa tuhuma zilizochochewa kisiasa. Serikali ya Kampala inakanusha tuhuma hizo.
Januari mwaka jana, 2024, Mahakama ya Juu ya Uganda ilitoa uamuzi unaopiga marufuku jeshi kuwahukumu raia.
Uamuzi huo uliilazimisha Serikali kuhamisha kesi ya mwanasiasa wa upinzani aliyekuwa mgombea urais, Kizza Besigye na kuipeleka katika mahakama za kiraia.
Besigye, ambaye ni mpinzani mkongwe wa kisiasa wa Rais Museveni, amekuwa kizuizini kwa takriban miezi mitano kwa kile wanasheria wake wanasema ni mashtaka ya kisiasa.
Alizuiliwa katika nchi jirani ya Kenya mwezi Novemba na baadaye kuhamishiwa Uganda, ambako alishtakiwa katika mahakama ya kijeshi kwa kumiliki silaha kinyume cha sheria na makosa mengine.
Sasa, Besigye anaweza kukabiliwa na waendesha mashtaka wa kijeshi kwa mara nyingine tena kwa sababu ya sheria mpya ambayo serikali inapanga kuanzisha.
Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba wa Uganda, Nobert Mao, aliliambia Bunge jana Alkhamisi kwamba sheria hiyo imetungwa na inasubiri kuidhinishwa na baraza la mawaziri kabla ya kuwasilishwa bungeni
Alisema sheria hiyo itafafanua "mazingira ya kipekee ambayo raia anaweza kuwa chini ya sheria za kijeshi."