Watu 11 wauawa katika shambulizi jipya jimboni Benue, Nigeria
(last modified Wed, 23 Apr 2025 10:59:15 GMT )
Apr 23, 2025 10:59 UTC
  • Watu 11 wauawa katika shambulizi jipya jimboni Benue, Nigeria

Watu wasiopungua 11 wameuawa kufuatia shambulizi jipya lililofanywa na wafugaji wenye silaha katika jamii ya Afia, iliyoko katika eneo la Serikali ya Mitaa ya Ukum, Jimbo la Benue, kaskazini-kati mwa Nigeria.

Tukio hilo limetokea chini ya siku tano baada ya mauaji ya zaidi ya wakulima 50 katika jimbo hilo.

Kwa mujibu wa Iyorkyaa Kaave, kiongozi wa jamii iliyoathirika, shambulizi hilo lililotokea Jumanne alasiri lilikuwa “bila kichocheo na ni sehemu ya mpango wa makusudi wa kuwafukuza wakulima wa jadi kutoka maeneo yao.”

Amesema  shambulizi hilo dhidi ya Afia lilikuwa la kikatili mno, kwani washambuliaji waliojizatiti kwa silaha walivamia jamii hiyo na kufyatua risasi kiholela na kusababisha vifo vya watu 11 papo hapo, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Eneo la kaskazini-kati mwa Nigeria limekuwa likishuhudia ongezeko la ghasia kati ya wakulima na wafugaji katika miezi ya hivi karibuni. Mashambulizi hayo katika jamii mbalimbali yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 100 ndani ya kipindi cha wiki mbili pekee.

Mgogoro kati ya wakulima na wafugaji nchini Nigeria ni miongoni mwa changamoto kubwa zaidi zinazolikabili taifa hilo katika miaka ya hivi karibuni. Chanzo cha mzozo huo ni mivutano juu ya umiliki wa ardhi na vyanzo vya maji, pamoja na masuala ya kuingiliwa kwa njia za jadi za uhamaji, wizi wa mifugo, na uharibifu wa mazao.

Msemaji wa polisi wa Jimbo la Benue, Sewuese Anene, amesema kuwa juhudi za kurejesha hali ya utulivu katika jamii ya Afia zinaendelea. Hata hivyo, wakazi wameiomba serikali ya Rais Bola Tinubu kuchukua hatua madhubuti na kuonya dhidi ya jaribio lolote la kujadiliana na wahusika wa mauaji hayo.