Uganda yatangaza kumalizika mripuko wa karibuni wa ugonjwa wa Ebola
Uganda imetangaza kumalizika mripuko uliozuka karibuni zaidi wa ugonjwa wa Ebola miezi mitatu baada ya mamlaka husika kuthibitisha kesi za maambukizo ya ugonjwa huo katika mji mkuu Kampala.
Wizara ya Afya ya Uganda imeeleza kwenye ujumbe uliowekwa kwenye mtandao wa X: "habari njema! Mripuko wa sasa wa ugonjwa wa Virusi vya Ebola Sudan umefikia kikomo rasmi".
Taarifa hiyo imeongezea kueleza kwamba, uamuzi huo umetangazwa baada ya kupita siku 42 "bila kesi mpya tangu mgonjwa wa mwisho aliyethibitishwa kuruhusiwa."
Nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilitangaza mripuko wake wa hivi punde Januari 30 baada ya kifo cha muuguzi wa kiume ambaye alipimwa na kukutwa na virusi hivyo.
Hata hivyo tangazo hilo la wizara ya afya ya Uganda haikutoa takwimu za jumla ya kesi zilizorekodiwa wakati wa mripuko huo.
Maambukizi ya Ebola yanatokea mara kwa mara nchini Uganda ambayo ina misitu mingi ya kitropiki ambayo ni hifadhi za asili za virusi vya ugonjwa huo.
Mripuko wa hivi punde, uliosababishwa na aina ya virusi vya Sudan ambayo haina chanjo iliyoidhinishwa, ulikuwa wa tisa nchini Uganda tangu nchi hiyo iliporekodi maambukizi yake ya kwanza mnamo 2000.
Ebola huambukizwa kwa kugusana na majimaji ya mwili na tishu zilizoambukizwa. Dalili zake ni pamoja na maumivu ya kichwa, kutapika damu, maumivu ya misuli na kutokwa na damu.../