Jeshi la Burkina Faso lazuia jaribio la kumpindua Traore
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125540-jeshi_la_burkina_faso_lazuia_jaribio_la_kumpindua_traore
Burkina Faso imethibitisha rasmi kwamba kulitokea jaribio la kuimpindua serikali ya nchi hiyo ambayo iko mstari wa mbele wa kuleta marekebisho ya kiuchumi kwa maslahi ya wananchi na dhidi ya madola ya kibeberu.
(last modified 2025-04-23T07:30:37+00:00 )
Apr 23, 2025 07:30 UTC
  • Jeshi la Burkina Faso lazuia jaribio la kumpindua Traore

Burkina Faso imethibitisha rasmi kwamba kulitokea jaribio la kuimpindua serikali ya nchi hiyo ambayo iko mstari wa mbele wa kuleta marekebisho ya kiuchumi kwa maslahi ya wananchi na dhidi ya madola ya kibeberu.

Tangu mapinduzi ya Septemba 2022 yaliyoongozwa na Kapteni Ibrahim Traoré, taifa hili la Afrika Magharibi limekuwa likiongozwa na utawala wa kijeshi ambao unaungwa mkono na wananchi. 

Kapteni Traoré mara kadhaa ameituhumu Côte d'Ivoire kwa kuwapa  hifadhi wapinzani wake.

Waziri wa Usalama wa Burkina Faso, Mahamadou Sana, amesema katika taarifa ya televisheni kuwa vyombo vya usalama nchini humo vimenasa mawasiliano kati ya afisa wa Jeshi la Burkina Faso aliyekuwa akivujisha taarifa za siri kuhusu jeshi.

Ameongeza kuwa njama hiyo kuu ilifikia kilele chake kwa mpango wa kushambulia ikulu ya urais mnamo Aprili 16, njama ambayo ilikuwa inatekelezwa na kikundi cha wanajeshi waliovutiwa na “maadui wa taifa.”

Sana amesema kuwa wapangaji wakuu wa njama hiyo wapo nje ya nchi na wanaendesha shughuli zao kutoka Côte d'Ivoire.

Ameongeza kuwa: “Njama hii inaendelea kutekelezwa kwa kasi kutoka kituo chao cha uendeshaji mjini Abidjan, kwa lengo la kusababisha vurugu nchini Burkina Faso kabla ya mwezi Juni."

Wiki iliyopita, maafisa kadhaa wa jeshi walikamatwa na kuondolewa kazini, hali iliyochochea uvumi kuhusu jaribio la mapinduzi ya kijeshi.

Serikali za kijeshi za Burkina Faso, Mali na Niger ziliunda Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) mnamo Septemba 2023 kupitia mkataba wa kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama miongoni mwa mataifa hayo matatu ya Afrika Magharibi.

Muungano huu wa kupinga ukoloni umechukua hatua madhubuti za kujitenga na ushawishi wa kikoloni, ikiwa ni pamoja na kujiondoa hivi karibuni kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) na Shirika la Kimataifa la Ufaransa (OIF). Mataifa haya pia yamesitisha makubaliano yote ya ushirikiano wa kijeshi na nchi za Magharibi, hasa Ufaransa na Marekani. Wachambuzi wanaamini kuwa mataifa ya Magharibi yanahusika moja kwa moja na njama za kuangusha serikali maarufu katika nchi hizo tatu.