Kutoweza Afrika Kusini kuachana na Muqawama na ukombozi wa Palestina
Tarehe 29 Disemba 2023 imerekodiwa katika kumbukumbu za historia ya baada ya mwaka 1994 ya Afrika Kusini kama siku muhimu sana baada ya Pretoria kufungua kesi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mahakama ya ICJ, ikiwasilisha hoja za kisheria za kina na zenye mashiko kwamba ukatili wa Israel katika Ukanda wa Ghaza unakanyaga Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari.
Kwa kuzingatia hatua hiyo ya kishujaa na ya kihistoria, wanasheria na wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, si rahisi kwa Afrika Kusini kuachana na suala la kupigania ukombozi wa Palestina na kuunga mkono Muqawama. Timu ya wanasheria wa Afrika Kusini, inayojumuisha wataalamu wa sheria za kimataifa imetilia mkazo jambo hilo na kusema kuwa Afrika Kusini haina njia nyingine isipokuwa kuendelea kuunga mkono Palestina. Aidha timu hiyo ya wataalamu wa sheria wa kimataifa, imeiomba Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi kuchukua maamuzi ya kiuadilifu ya kuwatendea haki Wapalestina ambao wamedhulumiwa vibaya katika kipindi cha zaidi ya miaka 75 na kukomesha uvamizi wa Israel kwenye ardhi za Wapalestina.
Juhudi za Afrika Kusini za kuongoza kesi dhidi ya utawala wa Kizayuni zilileta matumaini tarehe 26 Januari 2024 wakati mahakama ya ICJ ilipoiamuru Israel kuchukua hatua zote za kuzuia kufanyika kitendo chochote kilichopigwa marufuku kwenye Ibara ya II ya Mkataba wa Mauaji ya Kimbari, na pia kuchukua hatua za haraka na madhubuti za kuruhusu huduma za kimsingi zinawafikia kwa haraka wananchi wa Ghaza. Hata hivyo ukaidi wa dola pandikizi la Kizayuni linaloungwa mkono kwa hali zote na madola ya kibeberu duniani hasa Marekani, umezuia kutekelezwa amri hiyo ya mahakama ya ICJ kama ambavyo pia hata waranti wa kutiwa mbaroni viongozi wa Israel wanaotenda jinai unakwamishwa na madola ya kibeberu ya Magharibi.

Kwa upande wake, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Naledi Pandor amesema kuwa, ni wazi kwamba kushindwa kusitishwa mashambulizi ya kimbari ya Israel kwenye Ukanda wa Ghaza kumefichua mapungufu ya mifumo ya kisheria ya kimataifa na kumeibua upya udharura wa kufanyiwa mageuzi ya kimsingi taasisi za kimataifa hasa Umoja wa Mataifa.
Ijapokuwa kwa mujibu wa Jaji Hanqin Xue, suala la Palestina limekuwemo kwenye ajenda za Umoja wa Mataifa tangu kuasisiwa kwake, lakini mpaka leo hii umoja huo umeshindwa kuwasaidia wananchi wa Palestina wakiwemo wale wa Ukanda wa Ghaza kupata haki yao ya kujitawala.
Kwa mtazamo wa Jaji Xue, kuhakikisha Palestina inapata haki yake ya kujitawala ni jukumu la Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na chombo chake kikuu cha mahakama ambacho kinapaswa kuhakikisha kwamba watu wa Palestina wanalindwa chini ya sheria za kimataifa hususan mbele ya mauaji ya umati na uhalifu mkubwa wanaofanyiwa na Israel.
Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, Afrika Kusini haiwezi kuachia njiani jitihada ilizozianzisha za kupigania haki za Palestina kwa njia za kisheria na mahakama. Hasa kwa kutilia maani kwamba, pamoja na kuwa mahakama ya ICJ iliiamuru Israel kukomesha uvamizi wake wa kijeshi, kufungua kivuko cha Rafah kwa ajili ya kufikishiwa misaada wananchi wa Ghaza na amri nyingizo, lakini hakuna hata amri moja ya mahakama iliyotekelezwa. Hivyo timu ya wanasheria wa Afrika Kusini imesisitiza kuwa, lazima Pretoria iendelee kuweko kilingeni kuhakikisha mapambano dhidi ya madola vamizi yanaendelea hadi Palestina itakapojikomboa.

Tukirejea kwenye msimamo wa Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, Bi Naledi Pandor, alisema kwenye mahojiano aliyofanyiwa hivi karibuni kwamba anasikitika kuona kuwa bado dunia imeachiwa kuendelea kuwa na msimamo dhaifu kuhusu Palestina wakati watu wanaendelea kuuliwa kikatili.
Amesema: "Tunahitaji kuwa na nguvu za kijeshi ambazo zitaweza kwenda kuwa mlinzi wa watu wasio na hatia popote madhara kama hayo yanapotokea duniani."
Wataalamu wanasema kuwa, jukumu la Afrika Kusini hivi sasa ni kubwa zaidi hasa baada ya Donald Trump kurejea madarakani huko Marekani akiwa na dhamira yake potofu ya kuilinda Israel kwa hali yoyote ile hata kwa kuharibu uhusiano wake na mataifa mengine kama Afrika Kusini. Utawala wa Trump umeonesha wazi kuhamakishwa na hatua ya Afrika Kusini ya kufungua kesi dhidi ya Israel kwenye mahakama ya ICJ na inaishinikiza Afrika Kusini ifute kesi hiyo.
Timu ya wanasheria ya Afrika Kusini pia imesema kuwa, Pretoria haina budi ila kuendelea kujitolea kwa maadili ya haki za binadamu kuitetea Palestina na si kwa kiwango cha serikali tu, bali pia kuwahamasisha wananchi wake kutoshirikiana kivyovote vile na utawala wa Kizayuni bali kushirikiana kwa pamoja katika kuendeleza historia ya Afrika ya Kusini ya kuwa pamoja na Palestina katika hali zote.