Waziri: Kukubaliwa Uganda kuwa mshirika wa BRICS ni hatua muhimu
(last modified Fri, 02 May 2025 02:49:36 GMT )
May 02, 2025 02:49 UTC
  • Waziri: Kukubaliwa Uganda kuwa mshirika wa BRICS ni hatua muhimu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda, Jeje Odongo amesema kukubaliwa nchi hiyo kuwa taifa mshirika wa BRICS kunaashiria hatua muhimu katika uhusiano wa kigeni, na matarajio ya maendeleo ya nchi hiyo.

Odongo amesema Uganda sasa inaungana na kundi la nchi zenye malengo ya pamoja huku zikipigania kwa pamoja ustawi na maendeleo endelevu.

"Ni hatua kubwa kwa Uganda, ambayo inajivunia uhusiano thabiti na nchi wanachama na washirika wa BRICS, na ina mambo mengi yanayowaleta pamoja. Uganda imejitolea kuwa na mchango athirifu kwa malengo ya BRICS," Odongo amesema.

"Tunashukuru nchi wanachama waanzilishi kwa kufungua BRICS na kuruhusu wanachama wapya na washirika kujiunga na jumuiya hiyo. Ubadilishanaji huu ni ishara kubwa kwamba BRICS inafaa, na itaendelea kuwa muhimu na kukua duniani kote," Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda ameeleza.

Odongo ameieleza BRICS kama sauti kubwa katika eneo la Kusini mwa Dunia, katika ulimwengu unaozidi kuwa na mgawanyiko, ambapo jukumu la umoja wa pande nyingi liko chini ya tishio.

"Katika hali ambayo dunia inakabiliwa na changamoto kubwa za kijamii, kiuchumi na kijiografia, changamoto hizi huongeza hitaji kubwa la jumuiya tofauti kama BRICS kusimama kidete kama sauti ya eneo la Kusini mwa Ulimwengu," ameongeza Odongo.

Tokea Januari 1, mwaka huu 2025, Uganda iiliidhinishwa rasmi kuwa nchi mshirika wa BRICS, ikijiunga na nchi nyingine nane katika jumuiya hiyo ya nchi zinaoinukia kiuchumi duniani. Ikumbukwe kuwa, Oktoba 2024 katika mkutano wa kilele wa BRICS uliofanyika huko Kazan, nchini Russia, iliamuliwa kuundwa kikundi cha nchi "washirika wa BRICS".