Museveni: Kushiriki kwetu kumesaidia kushindwa waasi Sudan Kusini na DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126044-museveni_kushiriki_kwetu_kumesaidia_kushindwa_waasi_sudan_kusini_na_drc
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa operesheni za pamoja za kijeshi zilizoanzishwa na Kampala katika nchi jirani za Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimewashinda waasi katika nchi zote mbili.
(last modified 2025-05-05T23:15:04+00:00 )
May 05, 2025 23:15 UTC
  • Museveni: Kushiriki kwetu kumesaidia kushindwa waasi Sudan Kusini na DRC

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa operesheni za pamoja za kijeshi zilizoanzishwa na Kampala katika nchi jirani za Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimewashinda waasi katika nchi zote mbili.

Katika taarifa yake iliyotumwa kwenye akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa X Museveni amesema kwamba Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), limeyasaidia majeshi ya majirani hao wawili kuwashinda waasi.

Amesema kuwa, huko nchini DRC, UPDF imefanikiwa kukishinda kikosi cha Allied Democratic Forces (ADF) kwa msaada wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mwezi Machi, Uganda ilipeleka wanajeshi nchini Sudan Kusini huku hali ya wasiwasi ikiongezeka kati ya vikosi vinavyomtii Rais Salva Kiir na vile vinavyomtii Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar.

Huko nchini DRC, wanajeshi wa Uganda na wenzao wa DRC walianza operesheni ya pamoja dhidi ya waasi wa ADF mwezi Novemba 2021, muda mfupi baada ya kundi hilo la waasi kuanzisha mashambulizi ya mabomu huko Kampala, mji mkuu wa Uganda.

Genge la waasi la ADF ambalo ni kundi la waasi wa Uganda ambalo limejikita katika misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kundi hilo la waasi linalaumiwa kwa kusababisha uharibifu mkubwa katika vijiji vya mashariki mwa DRC.

Mapema mwaka huu, Uganda ilipeleka wanajeshi huko Ituri ili kuzuia mashambulizi ya wanamgambo wenye silaha wa Lendu wanaoendesha shughuli zao chini ya waasi wa CODECO na wanamgambo wengine.