Serikali ya Tripoli yapinga kupelekwa Libya wahamiaji kutoka Marekani
(last modified Thu, 08 May 2025 07:06:14 GMT )
May 08, 2025 07:06 UTC
  • Serikali ya Tripoli yapinga kupelekwa Libya wahamiaji kutoka Marekani

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imepinga vikali mpango wowote wa kupokea wahamiaji haramu waliofukuzwa kutoka Marekani.

Serikali hiyo inayotambuliwa kimataifa jana Jumatano ilisisitiza kuwa, haiafiki mpango wa nchi yoyote inayotaka kuitumia Libya kama kimbilio la wahamiaji waliotimuliwa bila ya wao kuarifiwa au kuafiki, na imejitolea kwa dhati kulinda mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.

Serikali hiyo yenye makao yake makuu mjini Tripoli imesema katika taarifa iliyosambazwa kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook kwamba, inapinga kikamilifu mpango wowote wa kuwapokea wahamiaji walotimuliwa Marekani bila ridhaa za wahajiri hao.

Kauli hiyo imekuja baada ya vyombo kadhaa vya habari vya Magharibi kama Reuters, BBC, CNN, na The New York Times, kuripoti kuwa Washington inapanga kuwasafirisha wahamiaji haramu katika nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika.

Kutokana na ukosefu wa usalama na machafuko nchini Libya tangu kuangushwa kwa serikali ya Muammar Gaddafi mwaka 2011, idadi kubwa ya wahamiaji, aghalabu yao wakiwa Waafrika, hukhitari kuvuka Bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya kupitia Libya.

Hivi sasa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imeongeza juhudi za kukabiliana na suala la uhamiaji haramu na magendo ya binadamu. Kwa mujibu wa Karoline Leavitt, Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House ya Marekani, katika miezi michache ya kwanza ya urais wa Donald Trump, maelfu ya wahamiaji haramu wamekamatwa na kuzuiliwa, huku wengine wakifukuzwa nchini humo.

Moja ya ahadi kuu za kampeni za Donald Trump wakati wa uchaguzi wa urais wa 2024 ilikuwa kuzuia wahamiaji haramu kuingia nchini Marekani.