Rais wa Algeria asema nchi yake haitasahau uhalifu wa ukoloni wa Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126150-rais_wa_algeria_asema_nchi_yake_haitasahau_uhalifu_wa_ukoloni_wa_ufaransa
Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria, amesisitiza kwamba suala la kumbukumbu ya kitaifa kuhusiana na utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini humo “halitakuwa jambo la kusahauliwa au kukanwa.”
(last modified 2025-05-08T07:26:17+00:00 )
May 08, 2025 07:26 UTC
  • Rais wa Algeria asema nchi yake haitasahau uhalifu wa ukoloni wa Ufaransa

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria, amesisitiza kwamba suala la kumbukumbu ya kitaifa kuhusiana na utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini humo “halitakuwa jambo la kusahauliwa au kukanwa.”

Matamshi ya Tebboune yalitolewa Jumatano katika hotuba kwa taifa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 80 ya mauaji ya Mei 8, 1945, yaliyotekelezwa na serikali ya kikoloni ya Ufaransa, ambapo waandamanaji 45,000 waliuawa wakiwa wanadai Ufaransa itimize ahadi yake ya kuwapa uhuru baada ya Waalgeria kuisaidia wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Tebboune amesema: “Maandamano ya Mei 8 yalionyesha kwa dhati mshikamano wa watu wa Algeria na hamu yao ya kupigania uhuru, heshima na fahari, walipokabiliwa na moja ya mauaji ya kimbari na uhalifu mbaya zaidi dhidi ya binadamu katika historia ya sasa, wakitoa zaidi ya mashujaa 45,000 kwa ajili ya uhuru na ukombozi."

Katika maadhimisho hayo, Tebboune amerudia msimamo wa Algeria kuhusu kushughulikia suala la nyaraka za kihistoria, jambo ambalo limekuwa chanzo cha mvutano wa muda mrefu na Paris, akisisitiza: “Suala la kumbukumbu halitakuwa jambo la kusahauliwa au kukanwa.”

Amethibitisha kwamba “kutoachia suala hili kunatokana na kufungamana na malengo ya mashujaa wa mauaji yaliyotekelezwa na mkoloni  Mfaransa nchini Algeria,” hasa katika majimbo ya Setif, Kherrata na Guelma Mashariki, Ain Temouchent Magharibi, na maeneo mengine, ambako maelfu kwa maelfu ya raia waliuawa katika moja ya uhalifu mbaya zaidi wa kikoloni.

Amesisitiza kuwa kujitolea kwa watu wa Algeria wakati wa vita dhidi ya  ukoloni kunahusiana moja kwa moja na dhamira ya sasa ya taifa ya kujenga mfumo endelevu wa maendeleo unaolinda uhuru wa kitaifa na maamuzi ya kujitegemea.

Vyanzo vya kihistoria vinaonyesha kwamba mauaji ya Mei 8, 1945 yalidumu kwa zaidi ya siku 40, ambapo majeshi ya kikoloni yalitumia mbinu za ukandamizaji za kikatili, ikiwa ni pamoja na mauaji ya halaiki na kuwachoma raia wakiwa hai ndani ya “tanuri za chokaa.”

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika huku mvutano katika uhusiano wa Algeria na Ufaransa ukiongezeka, na kufikia hatua ya kuondoa mabalozi na kufukuza wanadiplomasia, huku migongano kuhusu kumbukumbu na historia ya ukoloni ikiendelea.