DRC: Chama cha Kabila chasema kimerejea kazini licha ya kupigwa marufuku
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126160-drc_chama_cha_kabila_chasema_kimerejea_kazini_licha_ya_kupigwa_marufuku
Chama cha Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila kimesema kuwa, kitaendelea na shughuli zake kama kawaida licha ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo kupiga marufuku shughuli zake hizo.
(last modified 2025-05-08T22:51:39+00:00 )
May 08, 2025 22:51 UTC
  • DRC: Chama cha Kabila chasema kimerejea kazini licha ya kupigwa marufuku

Chama cha Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila kimesema kuwa, kitaendelea na shughuli zake kama kawaida licha ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo kupiga marufuku shughuli zake hizo.

Agizo la serikali la kupiga marufuku shughuli za Chama cha People's Party for Reconstruction and Democracy (PPRD) halijaondolewa. Lakini mawakili wa chama hicho wanahoji kuwa vipi agizo hilo litaendelea kuwa na nguvu bila ya idhini ya mahakama? Kwa mujibu wa sheria, kusimamishwa huko kuliisha kwenyewe tu moja kwa moja baada ya siku 15.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya DRC iliyojaribu kuhalalisha kupigwa marufuku chama cha PPRD ilimtuhumu Joseph Kabila kuwa anashirikiana na waasi wa M23.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya DRC ilisema kuwa, Joseph Kabila mwenye umri wa miaka 53 amekuwa akisita kuilaani M23, kundi la waasi linalodhibiti majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) sambamba na kuilaani Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao.

Kinshasa inamtuhumu Joseph Kabila, ambaye yuko uhamishoni tangu mwaka 2023, kuwa anashirikiana na madola ya kigeni kuunga mkono uasi wa kutumia silaha mashariki mwa nchi hiyo.

Mwezi uliopita wa Aprili, Kabila ambaye alitawala DRC hadi mwaka 2019 alirejea katika siasa za nchi hiyo kwa matawi ya chini na aliingia kwa siri nchini humo.

Taarifa za vyombo vya habari zinasema kuwa Joseph Kabila alifika katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Goma kupitia Rwanda. Ingawa hata hivyo, Kabila hajaonekana tena hadharani tangu wakati huo.