Utafiti: Lishe za magharibi zinawadhuru Waafrika
Utafiti wa hivi karibuni uliofanyika umebainisha kwa mara ya kwanza kwamba Waafrika wanaokumbatia lishe za Kimagharibi zenye vyakula vilivyosindikwa kwa wingi, sukari na mafuta, wanakabiliwa na kuongezeka kwa uvimbe mwilini (Inflammation), kinga dhaifu, na magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Kutokana na hali hiyo wataalamu wanatoa wito wa haraka wa kurejea kwenye lishe asilia ya Afrika ambayo ni tajiri kwa virutubisho.
Kwa mfano katika eneo la Kilimanjaro, nchini Tanzania, kuna ongezeko la vyakula vya viwandani lakini bado pia kuna wengi wanaotumia vyaklia asili vijijini. Utafiti mpya katika eneo hilo umeonyesha athari zilizofichika za mageuzi ya lishe kuelekea ile ya wazungu au Kimagharibi. Watafiti walifuatilia vijana walioacha kutumia lishe za mababu zao zilizojumuisha mbege iliyochachushwa, mboga za majani na nafaka zisizosindikwa, hadi vyakula vyenye kalori nyingi na sukari. Wale waliotumia lishe hizi za Kimagharibi walionyesha ongezeko la uvimbe mwilini na kushuka kwa kinga ndani ya wiki chache tu.
Hata hivyo, waliporejea kula chakula cha asili, miili yao ilipona kwa haraka: uvimbe ulipungua kwa kasi, na kinga iliimarika. Matokeo haya, yaliyochapishwa katika jarida la Nature Medicine, yanaonyesha kwamba urithi wa vyakula vya Kiafrika si kumbukumbu tu ya historia, bali ni suluhisho lenye nguvu dhidi ya kuongezeka kwa magonjwa yanayotokana na lishe duni.

Katika mahojiano na African Currents, Dkt. Godfrey Temba, mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Kikristo cha Kilimanjaro (KCMUC), alielezea matokeo ya utafiti wa timu yake kuhusu athari za kiafya za lishe za Kiafrika ukilinganisha na lishe za Kimagharibi.
Dkt. Temba amesema mradi huu uliwalenga vijana wa kiume wenye umri wa miaka 20 hadi 40 pekee. Kulingana na utafiti huo, wakati washiriki waliporejea kula lishe ya Kiafrika, kulionekana kushuka kwa haraka kwa viwango vya cytokines vinavyosababisha uvimbe, kuimarika kwa uwezo wa kupambana na vijidudu, na mabadiliko chanya katika vimeng’enya muhimu vya kimetaboliki.
Utafiti pia ulionyesha kwamba seli za kinga zilirudi kwenye usawa, na kupunguza uvimbe. Hii inaashiria kuboreshwa kwa kazi za kinga na afya ya kimetaboliki.
Dkt. Temba anasema kupuuza chakula cha asili cha Kiafrika ni kupoteza suluhisho rahisi na linalopatikana kwa urahisi dhidi ya kuongezeka kwa ugonjwa wa kisukari na magonjwa ya moyo. Aliongeza kwamba kufanya utafiti na kuweka kumbukumbu za faida za kiafya za lishe za Kiafrika ni muhimu katika kupambana na mlipuko wa magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika.