Ethiopia yaunda polisi wa baharini kulinda Bwawa la Renaissance
Ethiopia imetangaza kuunda kikosi kipya cha polisi wa baharini kitakachokuwa na jukumu la kuhakikisha usalama karibu na Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD).
Meja Escudar Burhan, Mkuu wa Idara ya Ukaguzi na Viwango ya Polisi ya Shirikisho amesema: "Hii ni hatua ya kwanza ya aina yake nchini, ambapo kikosi maalumu cha usalama kimeanzishwa kulinda eneo la maji ya bara."
Amesema sababu ya hatua hiyo ni kuanza kazi Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) na kujazwa kikamilifu eneo lake la jumla la takriban kilomita za mraba 1,680.
Ameongeza kuwa: "Kuna udharura wa kuandaa kikosi cha polisi chenye uwezo wa kulinda ziwa hili la kutengenezwa na kuzuia uhalifu wowote unaoweza kutokea katika eneo hilo."
Akihutubia Bunge la Ethiopia, Waziri Mkuu Abiy Ahmed amesema, "Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance sasa limejaa 100%, sawa na Bwawa la Aswan," na amewahakikishia wabunge kwamba Ethiopia "imechukua tahadhari zinazohitajika ili kuepuka kutatiza mtiririko wa maji kuelekea nchi nyingine za maporomoko ya maji ya Mto Nile."

Ujenzi wa bwawa hilo umeibua mvutano mkubwa wa maji kati ya nchi Ethiopia, Misri na Sudan tangu mwaka 2011 hadi sasa.
Misri na Sudan zinahofia kwamba bwawa hilo kubwa lililogharimu dola bilioni 4.2 litapunguza kwa kiasi kikubwa sehemu ya maji ya Mto Nile wanayopokea, na mara kadhaa zimeiomba Addis Ababa isitishe kulijaza hadi makubaliano yafikiwe.