Iran: Hatutakubali utwishaji wa Magharibi; tutaendelea kurutubisha urani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amepinga vikali mashinikizo ya nchi za Magharibi ya kuitaka Jamhuri ya Kiislamu iache kurutubisha madini ya urani, akiyataja mashinikizo hayo kuwa ni juhudi za kulitwisha taifa la Iran matakwa yao.
Araghchi amesema hayo alipofanya ziara katika Haram ya Imam Khomeini (MA), kusini mwa mji mkuu Tehran leo Jumamosi, ili kujadidisha utiifu wake kwa itikadi za Muasisi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu.
"Wakati pande nyingine zinaposema lazima tukomeshe urutubishaji, kimsingi zinajaribu kutwisha aina fulani ya utawala na ukuu wake juu yetu," amesema Araghchi.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza kuwa, "Chini ya sheria za kimataifa, tuna haki sawa na nchi nyingine yoyote ile kufaidika na teknolojia ya amani ya nyuklia, ikiwa ni pamoja na kurutubisha (urani)."
Araghchi pia amepuuzilia mbali eti wasiwasi wa nchi za Magharibi juu ya mpango wa kurutubisha urani wa Iran, akisisitiza kuwa hivyo ni vijisababu visivyo na msingi vya kujaribu kuinyima nchi hii haki yake ya kisheria.
"Wanasema usirutubishe urani kwa sababu tu wana wasi wasi. Lakini je, wasiwasi wao ni sababu halali ya kutunyima haki ya kisheria na halali?" Ameuliza Sayyid Araghchi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameonya kuwa, kukubali matakwa hayo ya Wamagharibi ni sawa na kukubali kutawaliwa na mataifa ya kigeni, jambo ambalo wananchi wa Iran hawawezi kulivumilia kamwe.
Viongozi mbali mbali wa Iran wanasisitiza kuwa, katu Jamhuri ya Kiislamu hitasalimu amri, na kulegeza msimamo kwa haki yake halali ya matumizi ya nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.