Kesi ya aina yake, mahakama Misri yamhukuru kiongozi mpya wa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i127042-kesi_ya_aina_yake_mahakama_misri_yamhukuru_kiongozi_mpya_wa_syria
Mahakama moja ya kiidara ya Misri, jana Jumamosi iliendesha kesi ya aina yake ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya Abu Muhammad al-Jolani, kiongozi wa utawala wa hivi sasa wa Syria akiwa hayupo mahakamani. Kesi hiyo inaweza kuwa hatua ya kwanza ya kuwawajibisha wahusika wa jinai za kivita nchini Syria.
(last modified 2025-05-31T22:51:24+00:00 )
May 31, 2025 22:51 UTC
  • Kesi ya aina yake, mahakama Misri yamhukuru kiongozi mpya wa Syria

Mahakama moja ya kiidara ya Misri, jana Jumamosi iliendesha kesi ya aina yake ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya Abu Muhammad al-Jolani, kiongozi wa utawala wa hivi sasa wa Syria akiwa hayupo mahakamani. Kesi hiyo inaweza kuwa hatua ya kwanza ya kuwawajibisha wahusika wa jinai za kivita nchini Syria.

Jana Jumamosi, kikao cha kwanza cha kesi hiyo kimesikilizwa bila ya Ahmed al-Shara kuwepo mahakamani. Kikao cha kusikiliza kesi ya mtuhumiwa huyo ambaye anajulikana pia kwa jina la Abu Muhammad al-Jolani, kilifanyika katika Mahakama ya Kiidara ya Haki (yaani Baraza la Jimbo) huko Misri.

Jambo hilo linachukuliwa kuwa ni hatua ya kimahakama ya aina yake kabisa ambayo haijawahi kutokea na inalenga kuwahukumu wale waliohusika na vitendo vya jinai na uhalifu wa mauaji ya kimbari dhidi ya makundi ya watu nchini Syria.

Kesi hiyo dhidi ya mkuu wa utawala wa hivi sasa wa Syria iliendeshwa jana kwa mujibu wa kesi iliyofunguliwa mahakamani hapo na Mohamed Abu Zeid, wakili wa Misri aliyebobea katika kesi za ukiukaji wa katiba.

Katika kesi hii, Abu Muhammad al-Jolani anatuhumiwa kufanya uhalifu dhidi ya binadamu na dhidi ya watu wa jamii za wachache za Alawi na Druze huko Syria.

Katika kesi hiyo, Ahmed al-Shara, kiongozi wa kundi la Hayat Tahrir al-Sham (Jabhatu al Nusra), yuko juu ya orodha ya washitakiwa wa vitendo vya uhalifu na anatajwa kuwa mhusika mkuu wa jinai zilizoenea dhidi ya raia katika mikoa mbalimbali ya Syria.

Al-Jolani, ambaye hapo awali alikuwa kamanda wa Jabhat al-Nusra, tawi la zamani la mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda alibadilisha njia yake ya kisiasa na kijeshi na kuandaa kikundi kipya kilichoitwa Hay-at Tahrir al-Sham kilichoundwa na walewale wapiganaji wa Jabhat al Nusra.